Lwandamina aifungia kazi Mbeya City

Dimba - - Jumatano - NA SAADA SALIM

SASA roho za mashabiki wa Yanga zimetulia, baada ya kupata taarifa za kocha wao mkuu, George Lwandamina, kurejea mzigoni kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa wiki hii.

Kocha huyo aliondoka nchini baada ya kumaliza mchezo wao dhidi ya Singida United, uliomalizika kwa suluhu ya 0-0 na ikasemekana hatarudi, hali iliyozua hofu kwa mashabiki.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, kocha huyo amewasili jana alfajiri na leo ataanza kazi ya kuwawinda Mbeya City.

"Kocha amewasili asubuhi leo ( jana), lakini hakuweza kufika mazoezini kutokana na uchovu wa safari, kwa taarifa alizoniambia ataripoti kesho (leo) na kuendelea na majukumu yake ya kazi," alisema Hafidhi. Alisema pia hata wachezaji walikuwepo katika kikosi cha timu ya Taifa watawasili leo na kujiunga na mazoezi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Yanga jana kilifanya mazoezi Uwanja wa Uhuru chini ya kocha msaidizi, Shadrack Nsajigwa na leo Lwandamina mwenyewe anaanza kuwavalia njuga wachezaji wake kuhakikisha wanaiadhibu Mbeya City.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.