Spurs uwanjani wana Pochettino, ofisini wana Levy

Dimba - - Special -

TOTTENHAM Hotspurs inaburudisha kuitazama ikicheza wakati huu. Inacheza soka murua.

Zile bao 3-1 ilizokutana nazo Real Madrid kwenye usiku wa Ulaya, hawakufungwa kwa kubahatisha. Walifungwa kiuwezo. Spurs wako vizuri sana hivi sasa.

Walichofanyiwa Madrid kwenye dimba la Wembley, ni maisha ya kawaida kwa Spurs siku hizi. Ndani ya Ligi ya Malkia wanafanya sana. Hivi sasa wanaogopwa na kila timu Uingereza na nje ya Uingereza.

Kuna kitu tunachomdai kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, juu ya Spurs hii na anapaswa kutulipa kitu hicho haraka iwezekanavyo kabla hajaachana na Liverpool na kuondoka Uingereza. Klopp ameitaja Manchester City kama timu iliyokamilika zaidi wakati huu nchini Uingereza, kuliko timu nyingine. Ina maana Klopp hajaiona Spurs au kiburi?

Aibu iliyoje siku tatu baada ya Klopp kufungwa mabao 4-1 na Spurs, ndiyo amekuja kutupa kauli hii inayotufikirisha zaidi kwenye mabongo yetu, lakini hatuipatii majibu stahiki. Hivi Klopp alimaanisha kusema vile au alitutania?

Kando ya City, Spurs ni timu nyingine ya kuogopwa. Kama huiogopi Spurs hii, utaiogopa Spurs gani nyingine? Klopp anapaswa kurudi tena kwenye vitonge vya waandishi na kuisawazisha kauli yake.

Kila wanalofanya Spurs wakati huu jeuri yao inatokana na wanaume wawili mashupavu. Mmoja anaitwa Daniel Levy anayeishi ofisini, mwingine anaitwa Mauricio Pochettino anayeishi uwanjani.

Wawili hao wameifanya Spurs iwe timu tishio kwa kila timu kubwa. Hivi sasa Chelsea, Madrid, Liverpool, zinakwenda kukutana na Spurs na hazijipi uhakika wa kushinda mechi. Maisha yameshabadilika.

Levy, Pochettino, wameifanya Spurs ifikie hatua hii ya kulitikisa soka la Ulaya tena kwa bei rahisi kabisa. Ndani ya uwanja wana Pochettino aliyeitengeneza timu imara inayomvutia kila mtazamaji, nje ya uwanja wana Levy anayesaini hundi za mauzo ya wachezaji.

Levy na Pottchetino wametufundisha kitu. Wametufundisha kuwa sio ukiwa huna fedha ndiyo unashindwa kupata wachezaji wenye viwango cha dunia. Delle Ali, Harry Kane, Cristian Erinksen ni miongoni mwa vijana walionunuliwa kwa bei ndogo na kucheza soka la bei kubwa. Kane ndiyo namba tisa bora duniani hivi sasa.

Ndani ya misimu miwili iliyopita Spurs ndiyo timu iliyominyana na timu za Leicester City na Chelsea mpaka dakika za mwisho kuliwania taji la ligi. Timu hii inakuwaje kawaida kama alivyoipuuza Klopp na kuitaja City pekee?

Katika soka la kileo linalonuka fedha za mafuta ya Waarabu, ni kazi ngumu kuwa na timu ya aina ya Spurs inayofanya vyema bila kutumia gharama kubwa sokoni. Soka la kileo haliko tena kwenye ubahili, liko kwenye uwekezaji mkubwa, ajabu iliyoje Spurs wametupa timu imara na yenye bei ndogo.

Wakati huu ambao Kane na wenzake wanapiga mpira mwingi kwenye viwanja vya nyumbani na ugenini, Levy ni mtu anayebadili mikao yake ofisini akisubiri simu za matajiri wa klabu mwishoni mwa msimu.

Vigogo wote wakubwa wa soka barani Ulaya macho yao yote yako Spurs. Kwa vyovyote vile ukifika muda wa dirisha la usajili vikumbo havitaisha ofisini kwa Levy ambaye hajawahi kuuza mchezaji kwa bei ya hasara.

Anachokifanya Levy hivi sasa ni kupiga tu miruzi na kulisubiri kwa hamu dirisha la usajili. Anajua matajiri watampigia tu simu yake na kutaka wachezaji kutoka kwake na hapa ndipo anaporinga.

Mara kadhaa Levy amevikacha vikao vya matajiri vinavyosindikizwa na vikombe vya kahawa kuhusu majadiliano ya kuuza wachezaji. Hivi sasa anadengua sana. Ni yeye anayepanga dau la kuuza wachezaji wake na kama timu haijafikia dau analotaka anainuka kitini na kuondoka zake. Hivi sasa Levy amewagueza mateka matajiri wa Ulaya.

Madrid wameshaanza kusema wanamtaka Kane na dau lao la kwanza wameshaliweka wazi kuwa watatoa pauni milioni 180. Licha ya Madrid kuanza na dau hilo nono, lakini Levy ni kama hajawasikia vile.

Amekaa kimya kama hajui nini wanachokitaka Madrid kutoka kwao likikaribia dirisha kubwa la usajili. Muda huu ambao Spurs wako kwenye ubora wao mkubwa kuanzia uwanjani hadi ofisini, tunapaswa kuwaheshimu kwa mapinduzi yao. Tuwaache Spurs na watu wao wawili.

Pochettino Levy

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.