Siri iliyojificha ndani ya uwezo wa akina Xavi, Lampard na Pirlo

SIRI ILIYOJIFICHA NDANI YA UWEZO WA AKINA XAVI, LAMPARD NA PIRLO

Dimba - - Special - KELVIN LYAMUYA NA MITANDAO

TULIPOKUWA tukiwatazama viungo aina ya Andrea Pirlo, Xavi, Andrea Iniesta, Frank Lampard na Steven Gerrard, wengi wetu hatukujua hasa ni kitu gani kilichojificha ndani ya uwezo wao wa kulimiki dimba la kati kwa umahiri mkubwa katika vizazi tofauti vya soka.

Walitushangaza na kutuburudisha kwa wakati mmoja. Tulijiuliza ni nini kinachowafanya wacheze vizuri mno?

Majibu ya maswali yote hayo anayo Dokta Geir Jordet, raia wa Norway na mchezaji wa zamani wa timu inayoshiriki ligi ya daraja la chini, Strommen IF, kabla ya kuchukua kozi ya saikolojia na kuwa Profesa.

Kazi yake hasa ni kutafiti sababu za kisaikolojia zinazopelekea mchezaji akacheza kwa kiwango cha hali ya juu, mfano; ni vitu gani hasa hupelekea mchezaji akafikia na kukiendeleza kiwango hadi juu kabisa.

Aidha, aliangalia namna mchezaji anavyoweza kuzihimili hisia zake na kuwa mtulivu ili aweze kucheza kwa kiwango kizuri hata anapokuwa kwenye presha ya juu.

Wengi wetu tumekuwa tukiwashushia sifa kedekede wachezaji hawa lakini ukweli ni kwamba hakuna mwenye kufahamu jinsi vichwa vyao vilivyokuwa vikifanya kazi kwa muda mfupi na kutoka na kitu kitakachotushangaza.

Jordet utafiti wake ulianzia kwa wachezaji wa klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi, akishirikiana vyema na wafanyakazi wa klabu hiyo akiwa kama mtaalamu wa michezo katika taasisi ya Cruyff Football.

Kikubwa alichokuwa akikifuatilia ni uwezo wa kufanya maamuzi (art of decision-making).

Alichanganua mambo muhimu katika ufanyaji maamuzi ndani ya vipengele vitatu ambavyo hata sisi katika maisha ya binadamu huwa tunayafanya.

Mosi aliangalia uwezo wa kuitengeneza taswira ya mchezo ulivyo na kukusanya taarifa mbalimbali kwa kutumia njia ya ufahamu na kuzitumia kufanya maamuzi au kutengeneza picha ya kitakachotokea baada ya sekunde chache.

Jordet alianza utafiti wake akiwa na kamera yake na kazi moja tu aliyofanya ni kumrekodi mchezaji kwa dakika zote 90. Aliwarekodi zaidi ya wachezaji 250 kwa ukaribu na kugundua kuwa wachezaji hao hufanya vitu tofauti kabla hawajapokea mpira.

Ni masuala ya kiutaalamu zaidi haya.

Moja kati ya video zake alizorekodi, Jordet anayo ya kiungo mahiri wa Barcelona na Hispania, Iniesta, katika michuano ya Kombe la Dunia 2010 World Cup.

Alimrekodi kiungo huyo katika mchezo wa fainali sekunde 10 kabla hajafunga bao la ushindi: Iniesta alionekana kama mtu anayefikiria kitu fulani katikati ya uwanja.

Alikuwa akijikusanyia taarifa mbalimbali kutoka kila pembe aliyoitupia jicho.

Alichokuwa akikifanya Iniesta ni kuhakikisha macho yake yalikuwa yakinasa kila taarifa uwanjani.

Jordet aliitaja hiyo ni kama kianzio chake kabla hajaanza kufanya maamuzi, kabla ya kufanya chochote lazima ahakikishe taarifa zote alizozihitaji zimenasa kwenye retina ya jicho lake kwanza.

Lampard naye alikuwa na uwezo huo. Kitaalamu, Jordet alimtaja Muingereza huyo kuwa ni bora katika sekta hiyo.

Jordet alikuwa na video ya sekude 16 ikimwonesha Lampard katika mtanange baina ya Chelsea na Blackburn, Oktoba 2009 akiwa kwenye nusu ya upande wa timu pinzani anaonekana akiutazama kulia na kushoto na kusogea kwenye nafasi kabla ya kugeuza tena shingo yake pande mbili kama mtu asiyeelewa cha kufanya lakini kumbe ndio anatengeneza picha ya eneo na nini cha kufanya pale atakapokuwa na mpira.

Kwenye video hiyo, Lampard anaonekana akitazama huku na kule mara 10 ndani ya sekunde saba kabla hajapokea pasi, alipoipokea akainua uso na kumtoka mchezaji mmoja (ambaye alishamuona akija) na kumsogezea pande mwenzake aliyekuwa kwenye nafasi nzuri.

Jordet anaandika kwamba, katika muda wake wote wa kufanya utafiti huo, aligundua Lampard ndiye mchezaji aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuitengeneza/kuivumbua picha kichwani ya kitu gani atakachokifanya kwa usahihi, kuliko mchezaji yeyote wa Ligi Kuu England.

Kilichomfanya agundue hilo ni namna alivyozichanganua tabia kama ya Lampard kwa kusoma mwenendo wa mwili au kichwa na wapi uso wa mchezaji unapotazama (wakati huo akiwa hautazami tena mpira alionao mguuni), asilimia kubwa ya lengo lake likiwa ni kukusanya taarifa kabla hajafanya jambo sahihi akiwa na mpira huo.

Utafiti huo ulifanywa kwa wachezaji 64 kwenye zaidi ya mechi 118, ambapo alikusanya matukio 1,279 katika hizo mechi. Patamu hapo. Jordet anaandika kwamba, Lampard alikuwa na wastani wa 0.62 wa kukusanya taarifa kabla hajapokea mpira, huku Gerrard akimkaribia kidogo (0.61).

Mtaalamu huyo anaamini kwamba, wachezaji ambao muda wote huwa makini kujikusanyia taarifa mbalimbali ndani ya mchezo kabla ya kupokea mpira ndio hupiga pasi nyingi timilifu.

Yote hayo kumhusu Lampard, Jordet anasema kuwa ni kitu cha msingi sana kama kikifanyiwa kazi mara kwa mara ndani ya mechi za ushindani baada ya kukifanyia mazoezi kwa sababu upepo unaweza kubadilika ghafla na ndio maana viungo wa karibu ya Lampard walitamba kwa muda mrefu kwa sababu ya uwezo huo wa

kukusanya

taarifa ndani ya mchezo na kufanya makubwa dimbani. Kwanini anasisitiza hilo? Jordet anaendelea kuandika kwamba, aliwahi kumuuliza Lampard katika mkutano fulani kuhusu uwezo wake huo baada ya kumfanyia utafiti, lakini Lampard alijibu kwamba pengine alizaliwa nao.

Kitu ambacho Jordet anakitaja kama ni changamoto kwa wachezaji wakubwa wakiulizwa maswali ya namna hiyo hudai kwamba hawajui au wamezaliwa na uwezo huo.

Bahati nzuri, wakati Jordet akipiga soga na Lampard, aliibuka kocha Tony Carr ambaye alikuwa akiinoa akademi ya West Ham wakati huo Lampard bado akiwa mtoto anayeibukia kwa kasi.

Carr alikuwa akisikiliza kwa umakini maongezi yao lakini aliamua kuingilia kati na kukumbushia namna baba yake Lampard, Frank Lampard Senior alivyokuwa akimfokea mwanae kila mara katika mchezo wa kwanza wa Lampard kwenye timu ya watoto.

Baba yake alikuwa akikaa kwenye siti zilizo karibu katika kuhakikisha mwanae anamsikia vizuri. Kila mara alikuwa akimfokea na kumhimiza atengeneze picha kichwani mwake kabla hajapokea mpira ili aweze kufanya maamuzi sahihi," alisema Carr.

Lampard alikiri: "Ni kweli, alinipigia sana kelele na nilichokifanya ni kutii maagizo yake."

Hatimaye sasa Jordet akapata jibu alilolitaka. Kumbe Lampard alikuwa akihimizwa tu kuwa mchanganuzi mzuri wa taswira ya mchezo tangu akiwa mdogo na si tofauti na hapo. Na ndicho ambacho Jordet aliwafundisha hata watoto wa Ajax. Anaandika kwamba, aliwahi kuwaonesha video moja ya Pirlo alipokuwa akiichezea Juventus dhidi ya Torino mwaka 2012.

Mwaka huo Pirlo alikuwa akicheza msimu wake wa mwisho mwaka huo huku umri ukianza kumtupa mkono, miaka 35 juu ya ardhi ya muumba. Kasi yake ilikuwa ni ndogo si kama zamani lakini bado alikuwa makini uwanjani, akitazama huku na kule kabla hajaunasa mpira. Alikuwa akiunda taswira kichwani.

Na alipoupata alihamisha macho yake na kuangaza huku na kule tena akitafuta jibu la wapi apite nao au wapi aipeleke pasi ya mauaji.

Xavi yeye alikuwa na wastani mkubwa zaidi wa kukusanya taarifa na kuunda picha kichwani kabla ya kuunasa mpira (0.83).

Jordet aliitaja tabia ya Maestro ya kurudisha haraka pasi ilipotoka kama hajakusanya taarifa yoyote ili kuepuka kama chachu ya kumweka kwenye kundi la juu zaidi la viungo makini sana duniani.

Mwaka 2011, Xavi aliwahi kunukuliwa na gazeti la The Guardian akisema: "Siri kubwa ni kuwaza haraka sana, tazama nafasi zilizopo. Ndicho ninachokifanya, natafuta wapi ilipo nafasi natulia, naisubiri pasi huku tayari nikiwa na picha yangu kichwani na bado nikiwa natazama huku na kule. Je, hapa panafaa, hapana, naiweka pale.

“Kama hauchezi soka lazima utaona ni jambo jepesi, hapana. Ni muhimu sana kufikiria na kuvumbua namna utakavyocheza kabla hujaunasa mpira.”

"Sikuzaliwa na huu uwezo ila yote ni mafunzo ya Johan Cruyff. Alituasa tuhofie sana kuipoteza hii elimu kuliko kupoteza mechi,” anaongeza. Jordet anasema kwamba, wachezaji mahiri siku zote huwa hawapigi pasi kama hawaoni sehemu ya kuipeleka pasi, mara nyingi huwa na picha yao kichwani na pasi zao hufika kwa watu ambao sisi watazamaji ni mara chache kung’amua kama wangeipeleka pale. Ni siri iliyokuwa imejificha ndani ya uwezo wao.

LAMPARD

XAVI PI

RLO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.