Shupavu FC, Viwandani nguvu sawa Daraja la Tatu

Dimba - - Jumatano -

MABINGWA wa soka Mkoa wa Morogoro, Shupavu FC na timu ya Viwandani, zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 2-2 katika mashindano ya Ligi Daraja la Tatu.

Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Understia Ifakara Mjini, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko zilikuwa zimeshafungana bao 1-1 ambapo timu ya Viwandani ndio ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu za Shupavu FC katika dakika ya 16, bao lililofungwa na Kassim Mpuche.

Kufungwa kwa bao hilo, timu ya Shupavu ilikuja juu na kusawazisha katika dakika ya 20 kupitia kwa Bobrey Lukindo kwa kusindikiza wavuni baada ya kipa wa Viwandani kutema shuti kali.

Katika kipindi cha pili cha mchezo, mchezaji Mpuche aliiandikia bao la pili timu ya Viwandani FC katika dakika ya 70, jambo lililowafanya Shupavu kuongeza kasi na kufanikiwa kusawazisha katika dakika ya 88 kupitia kwa mfungaji, Harun Mnasi baada ya faulo iliyopigwa na Avinho Adam Usanga.

Shupavu FC imebakiza mchezo mmoja dhidi ya timu ya Wailers, ambao unatarajiwa kucheza leo katika Uwanja wa Inderstia Ifakara Mjini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.