NASEPA Ronaldo agomea mkataba mpya Madrid, aomba kuuzwa

Dimba - - Jumatano - MADRID, Hispania

NYOTA wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ni kama ana ‘hasira’ baada ya vyombo vya habari kuripoti kwamba, Mreno huyo ameukataa mkataba mpya na ameomba kupigwa bei mwishoni mwa msimu huu. Ronaldo ambaye hivi karibuni aliweka wazi nia yake ya kutoongeza muda katika mkataba wake wa sasa ambao unategemewa kumalizika mwaka 2021, aliaminika kudhamiria kuondoka Santiago Bernabeu katika majira yaliyopita ya kiangazi. Hata hivyo, wakati supastaa huyo akiamua kubaki Madrid, ripoti za jana zilidai kuwa Ronaldo hataendelea kuwepo ndani ya klabu hiyo mara baada ya msimu huu kumalizika. Mtandao wa Daily Mail ulimnukuu mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Hispania cha El Chiringuito, Edu Aguirre, ambaye alidai kwamba Ronaldo alimwambia Rais wa Madrid, Florentino Perez, juu ya uamuzi wake huo wa kutoitumikia tena klabu hiyo. Aguirre aliongeza zaidi kwa kusema kwamba, Ronaldo, 32, anataka kutimka ifikapo Juni 30 na kwa bei inayoeleweka.

Hata hivyo, ilisemakana kwamba Madrid wamelipiga chini ombi lake hilo na huenda staa huyo akakasirishwa zaidi.

Inaaminika kuwa, Ronaldo hajisikii kama anakubalika tena Madrid na ofa waliyomweka mezani ni ishara mojawapo kwamba klabu hiyo haimthamini tena.

Aguirre alisisitiza kuwa Ronaldo ni mshabiki wa kutupwa wa Madrid ‘Madridista’ na anawapenda mashabiki, lakini moyo wake umeshaamua kuwa aondoke baada ya kushindwa kuelewana na vigogo.

Mapema msimu huu Ronaldo aliwahi kunukuliwa kama ataongeza mkataba ambapo alisema: “Sihitaji kuongeza mkataba. Nimetosheka na mkataba nilionao.”

Msimu huu umekuwa mgumu kwa mshambuliaji huyo akiwa na bao lake moja tu la La Liga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.