'OH!'

TUNA INIESTA WA KUMKUMBUKA, CARRICK WA KUMLILIA

Dimba - - Mbele -

KUNA matukio mengi sana ya kukumbuka ukitajiwa jina la Andres Iniesta.

Fainali ya Kombe la Dunia, mwaka 2010. Usiku wa Mei 28, 2011, Sir Alex Ferguson alipotetemeka mikono pale Wembley.

Nini tena? Kupigiwa makofi ya heshima na mashabiki wa Real Madrid.Yako matukio mengi sana lakini kubwa kuliko yote ni hili, Iniesta ni mchezaji bora aliyekosa tuzo ya Ballon d’Or.

Dunia ya soka imechagua kumuaga Andres Iniesta kwa machozi ya mamba.Tunajua alichokosa na hakuna aliye tayari kumpatia.

Ndani ya nafsi zetu tunaamini Iniesta alistahili kuondoka Barcelona akiwa na Ballon d’Or mkononi, lakini hatujui tukaichukue kwa nani.

Twende kwa Cristiano Ronaldo? Hapana.Wapi kwingine? Kwa Lionel Messi? Huku ni pagumu zaidi.

Anatutesa sana Iniesta. Kumwambia tumeshindwa. Kumsaidia tumeshindwa pia.

Hivi karibuni nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos, alinukuliwa akisema kuwa,“Kama Iniesta angeitwa Andresinho, basi angebeba Ballon d’Or”.

Nilicheka sana. Alichokifanya ni kujificha kwenye kivuli cha mtoto mdogo. Kwa akili ya kawaida kabisa, unaelewa kuwa Ramos alikuwa anamaanisha kuwa Iniesta amekosa tuzo kwa sababu si Mbrazil.

Si kichekesho hiki! Kwa miaka yote ya ufalme wa Iniesta, hakuna Ballon d’Or iliyoenda Brazil. Isipokwenda Ureno, ingekwenda Argentina.

Kuna sababu ya msingi kabla ya kutazama uraia wa Iniesta. Alistahili kubeba Ballon d’Or mwaka gani? Ramos alitakiwa kujibu swali hili kwanza.

Tunachoweza kufanya kwa Iniesta ni kuikumbuka elimu yake uwanjani. Uwezo wake wa kupiga pasi na kukokota mpira. Zaidi ya hapo ni kujiumiza tu kimawazo.

Tumewaona viungo wa aina nyingi sana uwanjani lakini wa aina yake, tulianza kumwona kwake.

Tumeishi na Iniesta mmoja tu duniani. Hakuwepo kabla na sidhani kama tutapata mwingine baadaye.

Huyu ni Andres Iniesta. Lakini upande wa pili tuna sura ya Michael Carrick. Sidhani kama inatosha tukimkumbuka tu, huyu ni wakumlilia kabisa.

Kuna mahala tumemkosea Carrick. Tumemkosea sana. Ni wapi hapo? Turudi nyuma kidogo.

Miaka 12 iliyopita. Katika majira ya kiangazi mwaka 2006, Sir Alex Ferguson, alijikuta kwenye wakati mgumu zaidi kama kocha wa Manchester United.

Ilikuwaje? Fedha ya Roman Abromovich, ilianza kumvuruga kwa kasi sana. Misimu miwili mfululizo Chelsea walibeba taji la Premier League mbele yake.

Arsenal waliokuwa wametoka kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, walitoka Highbury na kuhamia katika uwanja mpya wa Emirates.

Liverpool baada ya kutengeneza historia Ulaya, walirudi nyumbani na kumaliza msimu na ubingwa wa FA.

Wapinzani wake wote walikuwa moto kweli kweli.Vipi kwa Manchester United? Hali ni mbaya.

Ulikuwa msimu wao wa tatu bila ubingwa wa Ligi Kuu. Ruud van Nistelrooy, aliondoka kwenda Real Madrid na kibaya zaidi, nyota wao wawili, Cristiano Ronaldo na Wayne Rooney, walikuwa kwenye bifu zito.

Katikati ya uwanja, nahodha wao wa muda mrefu, Roy Keane, alishaondoka klabuni. Nani mwingine? Paul Scholes, alikuwa nje akiuguza tatizo lake la macho.

Wachezaji wawili waliocheza eneo la kiungo msimu wa 2005-06 ni John O'Shea na Alan Smith. Hakika United ilihitaji utatuzi wa haraka.

Hapa, katika janga hili, Ferguson alikwenda sokoni na kumsajili mchezaji mmoja tu. Ndio, mmoja tu. Michael Carrick, kwa pauni milioni 18 kutoka Tottenham Hotspur.

Baada ya usajili huu, mwandishi mmoja wa England aliandika makala iliyosema; "Pirlo kwenye nyumba ya Gattuso."

Carrick si aina ya viungo waliozoeleka katika soka la England. Mwaka 2006, mashabiki wa Kiingereza walizoea vita ya Roy Keane na Patrick Vieira.

Carrick hakuwa na sifa hiyo. Si Keane wala Vieira. Si Steven Gerrard wala Frank Lampard. Ni mchezaji wa aina gani? Anafanya nini katikati ya uwanja?

Jibu ni rahisi sana. Carrick ni ubongo wa timu. Kiungo mwenye kipaji cha kusoma njia za mpira uwanjani na uwezo mkubwa wa kupiga pasi.

Ni yeye aliyeutengeneza upya mfumo wa United. Ni yeye aliyemtengeneza Paul Scholes bora zaidi uwanjani.

Miaka saba baadaye baada ya ujio wake, mpaka Ferguson alipotangaza kustaafu 2013, United walikuwa wamebeba mataji matano ya ligi, mara mbili wakimaliza nafasi ya pili, tena wakigombea taji mpaka siku ya mwisho.

Kombe moja la Ulaya na fainali mbili, zote walipoteza dhidi ya timu bora Ulaya, Barcelona ya Pep Guardiola.

Kwanini tunatakiwa kumlilia Carrick? Hakupata heshima katika ngazi ya taifa na klabu pia.

Leo ukiambiwa utaje wachezaji watatu bora katika kikosi cha United mwaka 2009, bila shaka utaanza na Ronaldo, Rooney kisha utamaliza kwa Carlos Tevev.

Na hata ukiambiwa uongeze wengine watatu, utakuja kwa Paul Scholes, Rio Ferdinand na Nemanja Vidic. Bado ni ngumu Carrick kuja kichwani kwa haraka.

Ni rahisi Edwin van de Sar kuheshimika na mashabiki wa United kabla ya Carrick. Fundi huyu wa mpira hakuonekana kama ana kazi kubwa uwanjani.

Nuksi hii ameendelea nayo hadi katika timu yake ya taifa. Carrick ni mchezaji wa kawaida sana katika historia ya soka England.

Kituko zaidi ni katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010, pale kocha wa England, Fabio Capello, alipomweka benchi Carrick na kumtumia Gareth Barry, tena akiwa hayuko fiti kwa asilimia 100.

Iniesta ana heshima yake mioyo ya wanasoka. Amekosa Ballon d’Or tu, mengine amepata.Yuko kwenye kikosi bora cha Ulaya na dunia kwa miaka 10 iliyopita.

Ni shujaa wa Hispania. Anaheshimika mpaka na wabishi wa Santiago Bernabeu. Kwanini imeshindikana kwa Carrick?

Hakustahili? Tunaweza kusema Iniesta ameumizwa na uwepo wa Ronaldo na Messi, lakini hatuwezi kusema lolote kwa Carrick.

Ameumizwa na Gareth Barry? Ni kweli Owen Hargreaves ni bora kuliko Carrick? Hapa Waingereza kwa makusudi waliamua kucheza na akili zetu.

Kila la kheri Iniesta. Kila la kheri Carrick. Mafundi wa mpira wenye hadithi mbili zisizofanana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.