Singida Utd yanogesha ubingwa Msimbazi

Dimba - - News - NA CLARA ALPHONCE, SINGIDA

MABINGWA wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wamezidi kudhihirisha kuwa ubingwa wao haukuja kwa bahati mbaya, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida United, mchezo uliochezwa Uwanja wa Namfua, mkoani humo.

Licha ya kwamba waliingia katika mchezo huo wakiwa tayari wameshatwaa ubingwa, Wekundu hao wa Msimbazi wameonyesha dhamira yao ya kumaliza Ligi bila kupoteza mchezo ili kuweka rekodi nyingine.

Katika mchezo huo, bao pekee la Simba, liliwekwa wavuni na mchezaji wao kiraka, Shomari Kapombe, kwa shuti kali katika dakika ya 23, baada ya mabeki wa Singida United kufanya makosa eneo la hatari. Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.

Kipindi cha pili Singida United ndio walioonekana kuutawala mpira kwa dakika zote 45, lakini washambuliaji wao walishindwa kutumbukiza mipira wavuni, mpaka dakika 90 zinamalizika, Simba waliibuka na ushindi huo wa bao 1-0.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Klabu hiyo, Hajji Manara, alikuwa kivutio kwa baadhi ya mashabiki, baada ya kushangiliwa alipoingia tu uwanjani kabla ya mchezo kuanza, hali iliyomfanya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Said Tully, kwenda kumchukua na kumpeleka jukwaani.

Mbali na hilo, baadhi ya wabunge ambao ni mashabiki wa Klabu ya Simba, nao hawakuwa mbali na eneo la tukio, kwani walikodi gari kutoka Dodoma mpaka Singida kushuhudia mtanange huo.

Katika mchezo huo, kikosi cha Singida United, kiliwakilishwa na Ally Mustapha, Miraji Adam, Shafiq Batambuze, Mariki Antiri, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Kenny Ally, Kambale Salita, Lubinda Mundia pamoja na Salum Chukwu.

Simba, ambao walikuwa wageni, waliwakilishwa na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Jonas Mkude, John Bocco, Laudit Mavugo/Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi.

LIGI KUU

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.