Ubingwa Simba ufungue njia kimataifa

Dimba - - News -

MASHABIKI wa klabu ya Simba wana kila sababu ya kufurahia ubingwa wa timu yao iliyoutwaa Jumatano hii, baada ya washindani wao Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Tanzania Prisons kwa kufungwa mabao 2-0. Tunawapongeza Simba kwa kupata nafasi hiyo waliyoipigania kwa takribani miaka mitano, tunaamini juhudi zao ndizo zilizowafikisha hapa. Simba ilipata ubingwa wake ikiwa imebaki na michezo mitatu, lakini ilikuwa tayari ina jumla ya pointi 65 ilihali Yanga iliyokuwa inafuata nyuma yao kuwa na pointi 49 tu ambazo hata ikishinda mechi zake zote tano zilizosalia haitafikisha idadi hiyo. Sisi Dimba kama ilivyo kawaida yetu ya kutoa pongezi kwa timu au mwanamichezo atakayefanya vizuri awe mmoja mmoja au timu, lakini pia tunachukua nafasi kama hii kutoa ushauri. Kwa Simba ambayo ni klabu kongwe nchini, iliyoanzishwa tangu mwaka 1936, tunaikumbusha dhima ya kujipanga ipasavyo na sasa ikiangalia michuano ya kimataifa ambayo kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiboronga. Tunajua kwamba timu ya Simba ina historia nzuri ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, hivyo tunaikumbusha kujipanga vizuri kuanzia sasa ili iweze kurudisha ile heshima ya kufanya vizuri kimataifa ambayo kwa muda mrefu imepotea. Dimba tunafahamu fika kwamba licha ya ubingwa huo, lakini bado ligi haijaisha na kwamba Simba ina michezo miwili sasa ili kufikia tamati ya michuano hiyo, lakini bado ina jukumu la kujipanga kwani ubingwa ndiyo tiketi adimu ya kushiriki michuano ya kimataifa ambayo Simba imeshaikamata mkononi. Tunawatakia sherehe njema za ubingwa!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.