TAMBWE KUONGOZA MAUAJI KWA RAYON

Dimba - - Front Page - NA EZEKIELTENDWA

MASHABIKI wa Yanga hawana budi kuanza kutabasamu kutokana na mfungaji wao mahiri, Amis Tambwe, kukabidhiwa jukumu la kuongoza mauaji dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Tambwe ambaye hana masihara linapokuja suala la kufunga mabao, amekuwa majeruhi wa muda mrefu lakini sasa anaonekana kurudi upya.

Tangu msimu huu uanze, Mrundi huyo amecheza mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Prisons, kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimkabili hali iliyowasababisha Yanga kuzidiwa ujanja na watani zao wa jadi Simba.

Hata hivyo, taarifa njema kwa mashabiki wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ni kwamba straika huyo yupo tayari kuwavaa Rayon leo usiku.

Yanga watakutana na Rayon Sports katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho.

Katika mchezo wao wa kwanza walikubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger ya nchini Algeria na leo watataka kurejesha heshima yao.

Katika mazoezi ya juzi na jana, kocha mkuu wa kikosi hicho, Zaher Mwinyi, alikuwa akiwafundisha vijana wake hasa safu ya ushambuliaji namna ya kupachika mabao, huku Tambwe akionekana kubebeshwa zaidi jukumu hilo.

Yanga wanaburuza mkia katika kundi lao la D wakiwa hawana pointi yoyote, huku USM Alger wakiongoza na pointi zao tatu, Rayon Sports wakiwa na pointi moja katika nafasi ya pili sawa na Gor Mahia ya Kenya waliopo nafasi ya tatu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.