Awapa Barcelona taji la kwanza Ligi Kuu

R ONALDO de Assis Moreira maarufu kwa jina la Ronaldinho, jina lake lilikuwa halikauki kwa mashabiki wa soka nchini Hispania mara baada ya kusajiliwa na Barcelona mwaka 2003.

Dimba - - Dimba Special -

Jina hilo lilikuwa linazungumzwa na kila timu nchini Hispania bila ya kujali upinzani, ni kutokana na ubora na ufundi wa mchezaji huyo ambaye aliweka historia ya pekee.

Wiki iliopita kwenye simulizi ya makala ya mchezaji huyo tuliona kuwa msimu wake wa kwanza haukuwa na mafanikio makubwa japokuwa aliweza kuifanya timu hiyo kumaliza nafasi ya pili.

Mchezaji huyo aliikuta Barcelona ikishika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi, lakini aliweza kupambana na kuifanya imalize nafasi ya pili, hivyo aliwaahidi mashabiki kwamba taji litafuata msimu unaokuja baada ya kuwazoea vizuri wachezaji wenzake.

Leo hii tunaangalia mchezaji huyo jinsi alivyopambana na kufanikiwa kuwapa Barcelona taji hilo na yeye kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa Fifa.

Msimu huo wa 2004, mashabiki wa Barcelona walikuwa na imani kubwa ya kutwaa ubingwa baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili, hata hivyo kikosi chao kilionekana kuwa na damu changa nyingi ambazo zinaweza kupigania ubingwa.

Msimu huo Gaucho alikuwa kwenye kiwango kizuri na alitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa na uwezo mkubwa wa kunogesha mchezo na kuwaamsha wachezaji wenzake pale wanapokuwa kasi imepungua.

Hadi msimu unamalizika Barcelona waliweza kushinda jumla ya michezo 25 sawa na wapinzani wao Real Madrid walioshika nafasi ya pili na Barcelona walifungwa jumla ya michezo minne wakitoa sare michezo tisa, hivyo waliweza kutajwa mabingwa wapya kwa tofauti ya pointi 4, ambapo walikuwa na 84 huku Madrid wakiwa na 80.

Barcelona ilionekana kuwa kama timu ya mchezaji mmoja, wachezaji wengi walikuwa na mchango mkubwa lakini muda wote alikuwa anatajwa Ronaldinho kutokana na jinsi alivyowateka mashabiki kwa kile alichokuwa anakifanya.

Baada ya michuano hiyo kumalizika, mchezaji huyo alitajwa kuwa mchezaji bora wa msimu kwa wachezaji wa kigeni. Tuzo hiyo ilitokewa na wasimamizi wa michuano ya Ligi Kuu nchini humo (La Liga), ambao waliianzisha tangu mwaka 1996 hadi 2010. Hata hivyo, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jina lake lilitawala kwenye midomo ya wengi hasa kutokana na kile alichokifanya kwa wapinzani wake Chelsea. Mbali na kutolewa mapema na Chelsea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, lakini mchezaji huyo alikuwa kama mfalme na wengi walitamani kumuona akimaliza michuano hiyo hadi hatua ya fainali ili waweze kuona mambo mengi kutoka kwake. Unajua nini alikifanya Ronaldinho katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea na kuwafanya baadhi ya walinzi wa timu hiyo kubaki midomo wazi.

Tukutane Jumatano ijayo katika muendelezo wa makala haya ya nguli wa soka Ronaldinho Gaucho, Maoni na Ushauri nicheki kwa namba 0714107464 au Email Badimchomolo@yahoo.com

Na Badi Mchomolo

Mfahamu Ronaldinho (13)

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.