YANGA KINACHOTOKEA NI KAMA KUTAZAMA BONGO MOVIE

MIAKA michache iliyopita, Watanzania wengi tulikuwa wapenzi kweli kweli wa filamu za Kitanzania. Wakati huo kidogo walionesha weledi angalau tulipata kile ambacho waliweza kuyaakisi maisha ya jamii yetu.

Dimba - - Dimba Special - NA NIHZRATH NTANI JNR

Ghafla, watu wapya wakaingia. Miaka michache baadaye, filamu zikaanza kuzalishwa kama uyoga. Hili halikuwa tatizo, tatizo ubora mbovu wa filamu hizo. Ni wakati huo sasa mapenzi ya Watanzania dhidi ya filamu za Watanzania wenzao zikahama. Kwanini mapenzi yalihama?

Katika mfumuko huo, filamu hizo zikatuletea watu wa hovyo hovyo. Mwishowe wakatupa filamu za hovyo. Watu wabovu huzalisha vitu vibovu.

Mpaka sasa, wadau wa tasnia ya filamu hawajui wapi walipokosea. Soko la filamu limekuwa mfu. Wamebakia kutapatapa. Bongo Movie ipo Yanga sasa.

HUHITAJI KUNUNUA FILAMU WAKATI HUU, YATAZAME YANAYOTOKEA YANGA

Yanayotokea Yanga si tu yanachekesha, kuhuzunisha bali pia wanapaswa waonewe huruma. Miaka mitatu ama minne iliyopita, niliwahikumueleza mtu fulani kuwa kuna kiongozi hafai kuwa Mwenyekiti wa Yanga.

Kwa wakati ule ulihitajika ujasiri kuyatamka maneno niliyoyatamka, tena mbele ya mwanachama lia lia wa Yanga. Mtu yule aliniona mimi kama mpuuzi tu ninayetumiwa na Simba ama wapinzani wa Mwenyekiti wao. Kwanini nilimpa kauli ile?

Chini ya uongozi uliopita, kipato cha Yanga kilimtegemea mtu badala ya mipango thabiti ya klabu kujitegemea kiuchumi. Fedha za mtu mmoja zikawalevya wana Yanga.

Masikini hawakujua kesho yake. Walitembea vifua mbele mitaani. Sasa yote yamebakia kuwa historia. Hayo mambo hayapo tena Yanga. Yanga imekuwa kama mtoto yatima, haina mbele wala nyuma.

Mashabiki hawajui nini kifanyike kuiokoa klabu yao, huku viongozi wakiwa wamepoteza dira na wakibakia kutosema ukweli. Wote wamebakia kuwa kama waliochanganyikiwa. Kipi kimewapata mashabiki wa Yanga kwa wakati huu?

Kihistoria, mashabiki wa Yanga si watu baridi kiasi hiki. Ukimya wa mashabiki na wanachama wa Yanga umeanza lini? Bila shaka, haya yanayotokea Yanga tunaweza kuita filamu hii kwa jina la 'Heka heka Jangwani.' Inatosha kutazama.

VIONGOZI YANGA NI TATIZO

Kuna wakati lazima tuseme ukweli. Viongozi walioko Yanga si tu hawafai, bali kuendelea kubakia madarakani mpaka muda huu. Wanasubiri nini kuondoka kwa kujiuzulu?

Ni aibu kwa hadhi ya klabu ya Yanga kulia ukata. Viongozi hawajui namna ya kupata fedha kutoka kwenye mamilioni ya wapenzi wake na kutumia nembo ya klabu kuvutia wadhamini.

Wanao wadhamini wakiwemo Sportpesa, Macron, Azam TV, Vodacom na maji ya Afya, lakini kila kukicha wanalia njaa. Pesa zao zinakwenda wapi? Je, viongozi hawa wapo kwa maslahi ya klabu au wao binafsi? Inaumiza ukifikiria.

Si Clement Sanga ambaye ndiye Mwenyekiti kwa sasa wala kamati yake, wakiwemo akina Salum Mkemi, Hussein Nyika na Katibu Mkuu, Charles Mkwasa, anayeweza kutokeza mbele ya hadhara na kusema ukweli ulio ndani yao. Wamebakia kudanganya tu.

Ukiangalia filamu za wachezaji wao majeruhi na madai yao ya mishahara kwa muda mrefu ndio utabakia kujiuliza, huu ukimya wa mashabiki wa Yanga umetoka wapi?

Kwa wakati huu viongozi hawa walipaswa kuwa wamekwishaachia madaraka. Ukweli wa wazi wameshindwa kuongoza timu.

Ndani ya dimba Yanga ni mbovu mno. Kwa sasa mazingira yanaifanya Yanga ifungwe kabla haijaingia uwanjani. Wako wapi waliokuwa wakiubeza uwezo wa George Lwandamina? Sasa tunaweza kukubaliana kuwa Yanga hii ilikuwa ikipata matokeo chanya kwa sababu ya uwezo na mbinu za Lwandamina pekee.

Ninapoitazama nafasi iliyopo Singida United kisha nikamfikiria kocha Hans Pluijm kama angelikuwapo kwenye benchi kwa wakati huu, Yanga ingekuwa nafasi ya ngapi?

Labda tungekuwa kwenye maombi ya Yanga kuinusuru na nafasi ya kushuka daraja. Ni mechi saba sasa hawajashinda tangu kuondoka kwa Lwandamina.

Upuuzi na ujanja wetu tukamlazimisha aondoke. Tunahitaji kumuomba msamaha Lwandamina huko aliko.

WAKO WAPI MOHAMED KIGANJA, MZEE AKILIMALI NA WENZAO KUJITOKEZA SASA?

Ni kama yanayotokea Yanga hawayaoni. Wako kimya kweli kweli. Ni kama wamekuwa vipofu kwa wakati huu. Miaka michache iliyopita, Yanga ilitaka kukodiwa kwa kipindi cha miaka 10.

Mohammed Kiganja kwa mwamvuli wa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo nchini (BMT), akazuia. Ni katika mkumbo huo huo walikuwapo mzee Ibrahim Akilimali na wenzake. Ndoto ya Yanga kwenda kwenye mfumo mwingine ikazimika. Labda tungekuwa tunazungumza mengine sasa.

Nilitegemea kuwaona akina Kiganja wakiwa bega kwa bega na Yanga kwa wakati huu, akiiomba Serikali kuisaidia. Pia, ni wakati huu watangazaji wetu wangekuwa mlangoni kwa mzee Akilimali kumsikia ana mawazo yapi kuhusu hali ya Yanga, ila nao wako kimya.

WANACHAMA WA SIMBA, MNAJIFUNZA HAYA YANAYOWATOKEA WENZENU?

Wakiwa wanasuasua huku wakipata vikwazo kutoka serikalini na baadhi ya wanachama wachache kuhusu kupinga kwa Mohamedi Dewji kutwaa hisa zenye thamani ya asilimia 51, wanapaswa kutambua kuwa mfumo wa maisha umebadilisha soka. Soka linahitaji watu wenye pesa. Kila kitu katika soka kinahitajika uwe na pesa. Bahati mbaya viongozi wetu wengi hawapo madarakani kwa malengo ya kuendeleza soka bali kwa maslahi yao. Haya ni matokeo ya wanachama fulani kuzalisha viongozi fulani wasio na uwezo. Inasikitisha. Hakika kuimba kupokezana. Wanachama wa Simba mnapaswa kutambua hilo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.