Ammy Ninje tuambie Kabwili amekukosea nini?

K OCHA kwenye timu ndiye bosi mkuu. Ndiye msimamizi wa kila kitu ndani ya timu, lakini pia ni mzazi ambaye anawaongoza watoto wake kuhakikisha kwamba wanafanya kile kinachotakiwa.

Dimba - - Dimba Special - 1$ $+$', .$.25(

Katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, kuna mpasuko baina ya kikosi na mashabiki wake.

Chanzo cha mpasuko huo ni kuwekwa kando kwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Ramadhani Kabwili, ambaye ni mzoefu kwenye michuano mikubwa ya kimataifa.

Kocha wa kikosi hicho, Ammy Ninje, ameshindwa kueleza sababu za msingi za kumfanya kumuweka pembeni Kabwili kwenye mchezo baina ya timu hiyo na Mali, ambaye ni mzoefu ikilinganishwa na Abdul Twalib, ambaye si mzefu.

Kimsingi ushindi wa Mali ni kama Kocha Ammy Ninje alikuwa amewatafutia jambo ambalo limezusha mgogoro baina ya Kocha na wapenzi wa soka katika Taifa la Tanzania.

Kimsingi hakuna anayeweza kumpangia kocha kikosi chake, lakini niseme jambo moja kwamba, maudhi haya kocha ameyataka, japo hatujui sababu za kuamua kuumiza mioyo ya Watanzania kwa kiwango hiki.

Nakumbuka baada ya kuwapo kwa mgogoro huo baina ya kocha na Kabwili, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliamua kuingilia kati jambo hilo na kuamua Kabwili arejeshwe kikosini.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Kabwili ni kipa mzoefu kwenye michuano mikubwa, kwani alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliosaidia Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.

Lakini pia kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’, Kabwili alicheza mechi zote za fainali hizo, japokuwa kikosi hakikufanya vizuri sana, lakini kulikuwa na jambo ambalo wachezaji walijifunza.

Kwa uzoefi huo huo wa michuano ya kimataifa, ndiyo sababu ilimfanya hata Kocha wa Yanga, George Lwandamina, kuamua kumpanga katika kikosi kilichocheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na Township Rollers ya Botswana.

Japokuwa Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1, lakini Kabwili alifanya kazi kubwa, hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa akicheza na wachezaji wazoefu na huenda akawa kipa mdogo zaidi kucheza kwenye michuano ya mwaka huu.

Haya yalikuwa ni mafanikio makubwa kwake, kwa maana hiyo, ilikuwa ni sababu tosha kwamba Kabwili alikuwa anastahili au viatu vilikuwa vikimtosha kuitumikia nchi yake.

Nyongeza ni kwamba, hata katika mchezo wa awali wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana baina ya Ngorongoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kabwili alifanya kazi kubwa na kuiwezesha leo hii Tanzania inapata nafasi ya kucheza na Mali.

Swali kubwa ambalo Watanzania wameshindwa kupatiwa majibu ni kwamba, nini hasa kilichopo baina ya kocha na mchezaji huyo? Kama kuna ugomvi tuambiwe ili tumuombee Kabwili msamaha.

Lakini kama ni mambo binafsi inafaa pia tuambiwe, ili mambo yaishe na tuendelee mbele. Matatizo ambayo Ngongoro inapitia kwa sasa katika kuitafuta nafasi hiyo ni jambo ambalo limewaumiza Watanzania wapenda soka.

Pia Kocha Ninje aelewe kwamba, timu hiyo si mali yake, bali ni mali yetu sisi Watanzania. Kwa sababu kuna mambo mengine hayahitaji kutumia nguvu wala akili ya chuo kikuu katika kuweza kupata usahihi wake.

Kama nchi tunahitaji mafanikio, hasa ikizingatiwa kwamba, kwa sasa Tanzania ina timu mbili tu zinazotafuta nafasi ya kucheza fainali za Afrika. Kwanza, Ngorongoro na ile ya wakubwa, yaani Taifa Stars.

Ni ukweli siopingika kwamba, Tanzania inahitaji mafanikio, lakini si kwa njia ambayo Ninje anataka kutupitisha, kiukweli hatuwezi kufika, kwa sababu ameshaonyesha udhaifu katika utendaji wake.

Haya yanayotukuta sasa, nayafananisha na nyakati zile alizokuwapo Kocha Marcio Maximo, ambaye ugomvi wake na Juma Kaseja ulitufanya kutokuwa na timu imara na kujikuta tukifungwa au kupoteza mechi muhimu.

Zama za Maximo naamini zimepita, na sasa tupo kwenye kizazi kipya ambacho kinahitaji mabadiliko ya kweli na kuachana na mambo ambayo hayawezi kuisaidia nchi.

Kwa sababu hiyo, namuomba Kocha Ammy Ninje kutuambia kama Watanzania nini kosa la Kabwili, ili tuweze kumsaidia kuomba msamaha kwa sababu inaonekana hata maagizo ya bosi wake, yaani Rais wa TFF, hayasikilizwi.

Tanzania ni yetu, ikiharibikiwa wote tunachekwa, kwa hiyo hakuna sababu ya kuchekwa kwa sababu ya sababu zisizokubalika, tuungane kwa ajili ya Tanzania. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.