TFF yamuomba Magufuli kuwakabidhi Simba kombe

Dimba - - News - NA CLARA ALPHONCE

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. John Magufuli, kuwakabidhi Kombe Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, timu ya Simba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya TFF, jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, alisema kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na shirikisho hilo, ndiyo sababu ya kuomba taji hilo kutolewa na Rais.

“Kwa sasa tunasubiri majibu ya Rais ikiwa atakubali ombi letu, lakini tulichukua uamuzi huu kutokana na ushirikiano wetu wa karibu na Serikali, ndiyo imetufanya kuandika barua kumwomba Rais Magufuli alikabidhi taji hilo kwa Simba.

“Endapo atakubali ombi letu, Rais ataanza kukabidhiwa Kombe la Cecafa la vijana walilolitwaa katika michuano iliyokuwa ikifanyika nchini Burundi,” alisema Karia.

Simba inatarajia kukabidhiwa taji hilo Jumamosi ijayo katika mchezo wa 29 wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Rais Magufuli pia atakabidhiwa Kombe la Vijana la ubingwa wa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Cecsfa) na timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, ambalo ililitwaa Aprili, mwaka huu, nchini Burundi.

Simba ilitangazwa rasmi mabingwa wapya, baada ya timu iliyokuwa mabingwa watetezi, Yanga, kuutema kwa kufungwa mabao 2-0 na Tanzania Prisons, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Wekundu hao wa Msimbazi wanaongoza msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 68 baada ya kucheza michezo 28 bila kupoteza mchezo, huku ikifikisha mabao 61 na kufungwa 13.

Timu hiyo inalitwaa taji hilo la 19 tangu kuanzishwa kwake na mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni msimu wa 2011/12, kabla ya kufanya hivyo msimu huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.