Ya Babu Seya hebu msikilize King Kiki-44

*Ajisalimisha hotelini baada ya kutoswa na mwenyeji wake

Dimba - - Dimba Special - NA JUMA KASESA

JUMAPILI iliyopita katika simulizi hii sehemu ya 43, mwanamuziki gwiji wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki', aliishia akisimulia alivyokwea pipa kwa safari kwenda barani Ulaya nchini Ufaransa, ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kwenda kununua vyombo vyake tayari kwa kuanzisha bendi yake. Kiki anatua Ufaransa na kujielekeza nyumbani kwa mwenyeji wake kupitia anuani aliyopewa lakini cha ajabu jamaa anajifanya hana taarifa zake zozote na hata mtu aliyemwelekeza pia hamfahamu kabisa. SASA ENDELEA…

Kulikuwa na kila dalili kabisa yule bwana niliyekwenda kwake kugonga mlango na kufunguliwa kisha kujieleza kwamba mimi ni mgeni wake, ndiye Alphonce haswa ambaye nilipewa anuani yake na Alex Alex.

Baada ya bwana yule kukana kufahamu chochote kuhusu ujio wangu, niliondoka na kwenda geti la nyumba ya tatu kutoka kwake na kugonga mlango ili kupata usahihi wa anuani niliyonayo kama nimekosea kama alivyosema Alphonce.

Nilibonyesha kengele ya mlangoni ndani ya dakika kama mbili geti dogo la nyumba hiyo lilifunguliwa na kisha kujitokeza kijana wa Kiafrika mwenye umri unaokaribiana na wangu na kisha kunisabahi kabla ya kuniuliza anisaidie nini.

Nilimweleza mimi ni mgeni kutoka Tanzania, nina adresi ya mwenyeji wangu anaitwa Alphonce lakini sijui ni nyumba gani anaishi hapa mtaani. Aliniomba karatasi yenye maelekezo ya mji, mtaa na namba ya nyumba niliyonayo ili aisome kwanza. Kwa bahati nzuri ile karatasi ilikuwa imeandikwa na jina la Alphonce.

Sekunde 30 baada ya kuisoma ile karatasi akasema ooh mbona ni geti lile pale lenye rangi nyeusi nyumba ya tatu kutoka hapa. Nilishtuka kidogo na yeye akawa kama amehisi kitu kwa namna nilivyobaki nimetumbua macho mara baada yeye kunielekeza.

Alivunja ukimya kwa kuniuliza mbona umeshtuka. Nilimweleza nyumba ile ndo nimetokea na kugonga mlango lakini kilichotokea ni mtu niliyemkuta pale na kujitambulisha kwake amesema hawamjui huyo mtu anaitwa Alphonce lakini pia hata mtaa nitakuwa nimepotea.

Mshtuko wangu wa mwanzo sasa ulihamia kwake. Alishangazwa na maelezo niliyompa kwamba nimekosea hadi mtaa. Yalikuwa maelezo ambayo yalimfanya anitupie swali akiniuliza kama nina hakika na hicho ninachomueleza. Nilisisitiza kuwa nyumba ile nimekwenda lakini muhusika niliyemkuta amekana kufahamu lolote.

Aliniomba nimueleze kwa kifupi wajihi wa mtu niliyemkuta pale. Nilimweleza kila kitu kwa usahihi mwanzo wa kufika kwangu mpaka kuondoka ili apate picha kamili ya tukio zima.

Aliniomba nisubiri dakika mbili na kuingia ndani kabla ya kutoka na kuomba tuongozane mimi na yeye hadi kwenye nyumba hiyo ili agonge mlango apate ukweli wa kile nilichomuelekeza. Tuliongozana hadi kwenye geti la nyumba ile na kuniomba nikae kwa pembeni kidogo ili agonge. Alifanya hivyo na dakika chache geti lilifunguliwa na uso wake ukakutana na yule bwana aliyekana kwamba yeye si Alphonce.

Uso wao ulipokutana wawili hawa walisalimiana kwa furaha na yule bwana aliyenikana kama si mwenyeji wangu akawa anamkaribisha ndani yule mtu niliyeongozana naye. Aligoma kuingia. Walikuwa wakifahamiana kupitia ujirani wao ingawa hawakuwa marafiki sana.

Alichokifanya ni kumwambia bwana Alphonce nimemleta mgeni wako huyu hapa nje. Nilishtuka yule bwana kuitwa jina lile lile nililoandikiwa kwenye karatasi ambalo alilikana. Kumbuka muda wote huo mawasiliano ya lugha niliyokuwa natumia ilikuwa ni Kifaransa.Miongoni mwa faida kubwa niliyokuwa nayo ni ujuzi wa kutumia lugha hiyo.

Yule bwana Alphonce alishtuka kuona ameletewa msala mzito. Alipatwa na fedheha kubwa kuona mtu aliyemkana haitwi jina lile amejua ukweli wote. Alipatwa na aibu kubwa baada ya mimi kujitokeza mbele na kubaini nimejua kama ni yeye.

Nilimwambia yule bwana niliyeongozana naye tuondoke kwani sina haja ya kufikia tena kwa Alphonce, kwani nimejiridhisha si mtu mwema kwangu.

Tuliongozana hadi kwake na kunitambulisha kwa familia yake kisha kumweleza mkasa mzima ulionipata. Mkewe alisikitishwa na kunipa pole. Nilimweleza yule bwana anitafutie hoteli nzuri ya bei rahisi. Baada ya muda mfupi tuliondoka na gari yake kuelekea mahali ambapo kulikuwa na hoteli kulingana na hitaji langu. Je, nini kiliendelea kwa King Kiki nchini Ufaransa? Alifanikiwa kupata vyombo? Usikose kusoma DIMBA siku ya Jumapili kuendelea kupata uhondo wa simulizi hii.. Kwa maoni na ushauri 0715-629298.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.