Kocha Yanga aishangaa TFF

Dimba - - News - NA CLARA ALPHONCE

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amelishangaa Shirikisho la soka nchini, TFF, kushindwa kuahirisha mechi za Ligi Kuu za Simba na Yanga ili kuipa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ muda wa kutosha kujiandaa na maandalizi yake.

Kikosi cha Taifa Stars tayari kipo kambini kikijiandaa na mchezo wao dhidi ya Cape Verde, utakaochezwa Oktoba 12, huku wachezaji wa klabu za Simba na Yanga wakitakiwa kuzitumikia klabu zao katika michezo ya mwishoni mwa juma hili.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za New Habari (2006) Ltd zilizopo Sinza Kijiweni, Zahera alisema ni vyema TFF ingeahirisha michezo hiyo ya Ligi Kuu kutokana na umuhimu wa mchezo wa kimataifa ambao ni wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika mwakani.

Alisema ili kupata muda wa kutosha, wachezaji hao walipaswa kuingia kambini mapema na kuanza maandalizi ya pamoja ili wawezi kufanya vyema kwenye mchezo ulio mbele yao.

“TFF walipaswa kuahirisha michezo ya ligi kuu kwa timu zilizo na wachezaji walioitwa kwenye timu ya Taifa, hii itasaidia kuwapa muda wa kutosha kujiandaa na mchezo wa kimataifa ambao una umuhimu mkubwa sana kwao na kwa Taifa kwa ujumla,” alisema Zahera.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Clifford Ndimbo, alisema mechi za mwishoni mwa juma zitaendelea kama kawaida na wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha timu ya kawaida watarejea kwenye vikosi vyao siku moja kabla ya mchezo.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC siku ya Jumamosi, huku Simba wakiikaribisha African Lyon siku inayofuata kwenye Uwanja wa Taifa.

SOKA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.