DONOA DONOA

Dimba - - Burudani - NA MAREGES NYAMAKA

EMMANUEL OKWI

STRAIKA wa Simba amemtaja kipa wa mahasimu wao wa jadi kisoka Yanga, Beno Kakolanya, kuwa ndiye aliyekuwa kikwazo kikubwa kushindwa kuzifumania nyavu za timu hiyo. Okwi anasema safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ilicheza kufa au kupona kusaka matokeo bora lakini bahati haikuwa yao.

MOHAMMED HUSSEIN

BEKI wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amesema mbinu walizotumia Yanga za kujilinda zaidi ndizo zilizowapa nafasi nyingi ya kutawala mpira ingawa bahati haikuwa upande wao. Tshabalala amekiri kuwa walitawala mchezo kwa muda mrefu lakini makosa madogo madogo ndiyo yaliwafanya kushindwa kuibuka na ushindi.

JUMA MWAMBUSI

KOCHA msaidizi wa Azam FC amewata waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu kuongeza jicho la umakini katika majukumu yao ili kuepusha lawama za mara kwa mara. Anasema katika mchezo uliopita dhidi ya Lipuli ambapo walitoka suluhu, mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo alishindwa kusimamia kanuni 17 za mchezo wa soka.

JAMHUR KIHWELO

KOCHA wa Dodoma FC amesema wamejipanga vyema kupata pointi tatu katika mchezo ujao wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Rhino Rangers, utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, mkoani Dodoma Jumamosi ijayo. Julio anasema kikosi chake kina kila sababu ya kupata ushindi katika mchezo huo baada ya kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Pamba.

PETER MHINA

KOCHA Mkuu wa Majimaji amewatuliza mashabiki wa timu hiyo kuwa kikosi chake kitacheza kufa au kupona msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania ili kutimiza ndoto za kurudi Ligi Kuu. Mhina anasema baada ya kuanza na ushindi katika ligi hiyo, sasa mambo yataendelea kuwa moto mpaka mwisho wa msimu.

DONALD NGOMA

STRAIKA wa Azam FC amesema amefurahia kurudi kwake uwanjani ambapo akili na mawazo yake kwa sasa ni namna ya kurejesha makali yake aliyokuwa nayo wakati yupo Yanga. Ngoma ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu akitokea Yanga, amesema anaendelea kumwomba Mungu amsimamie asipate majeraha kwani anataka kuonyesha thamani ya usajili wake Azam FC.

SHABAN KATWILLA

KOCHA wa Mtibwa Sugar amesema kwamba wao hawadharau mechi yoyote kwa sababu Ligi Kuu msimu huu ni ngumu na haitabiriki. Amesema kwao timu kama Biashara United ambayo ni wageni katika Ligi Kuu hawatathubutu kuibeza kwani kwenye soka lolote linatokea.

SUBIRA WAZIRI

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Vishale Tanzania (TADA), amezitaka timu kuthibitisha mapema ushiriki wao katika michuano ya Taifa Cup inayotarajiwa kufanyika Novemba 23-25 mwaka huu, jijini Dar es Salaam. Waziri anasema timu zinatakiwa kuthibitisha mapema ili kuweza kuwapa nafasi ya kusaka fedha za michuano hiyo kulingana na idadi itakayokuwepo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.