Wenye Lipuli yao wataka pointi tatu

Dimba - - News - NA MWANDISHI WETU, IRINGA

TIMU ya Lipuli ya mjini Iringa kwa sasa imejikusanyia pointi nane katika michezo saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyokwishacheza hadi sasa, idadi ambayo wenye timu yao wanasema ni ndogo.

Dimba jana lilivinjari eneo la Soko Kuu mjini Iringa na kukutana na mashabiki wengi, ambao wanazungumzia mwelekeo wa ligi hiyo na kudai kwamba bado wana imani na kikosi chao, lakini wanataka kuongeza juhudi ili kijiweke katika sehemu salama.

Mashabiki hao kwa nyakati tofauti wamelalamikia jinsi timu yao ilivyopoteza wachezaji wengi walioisaidia msimu uliopita, walipokwenda kujiunga na timu nyingine, lakini wamemtaka Kocha Mkuu, Selemani Matola, kukaza buti kuhakikisha timu inafanya vizuri.

Kwa kuanzia amsha amsha hiyo, mashabiki hao, wamesema wataanza kuujaza Uwanja wa Samora Oktoba 21, wakati kikosi chao kitakapoivaa Kagera Sugar.

Mchezo huo utapigwa baada ya ligi kusimama kupisha michezo ya kimataifa, ambapo Timu ya Taifa ya Tanzania itacheza na Cape Verde Oktoba 12 ugenini na kisha kurudiana Oktoba 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kikosi chake, Matola alisema kikosi chake kinampa matumaini ya kufanya vizuri hapo baadaye, kutokana na marekebisho atakayoyafanya katika safu ya ushambuliaji ili timu iweze kupata mabao.

Hadi ikikamilisha mechi hizo saba, Lipuli imeweza kushinda mechi moja tu, na kupoteza moja, huku ikitoka sare mechi tano.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.