DAWA YA MOTO...

Guardiola awapania Liverpool kinoma

Dimba - - Sport Pesa -

MANCHESTER City wanarejea kwenye Uwanja wa Anfield leo kwa mara ya kwanza tangu walipobugizwa mabao 3-0 na Liverpool, Aprili mwaka huu, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ulikuwa ni usiku ambao Kocha wa Man City, Pep Guardiola, alishuhudia timu yake ikichakazwa mapema kutokana na uamuzi wake wa kutumia mfumo tofauti na ambao alikuwa anatamba nao msimu mzima. Liverpool walifunga hayo mabao matatu ndani ya dakika 30 za kwanza, Mohamed Salah, Alex Oxlade-Chamberlain na Sadio Mane wakihusika katika adhabu hiyo nzito kwa vijana wa Guardiola. Ni miezi sita sasa imeshapita, ukiwa ni muda wa kutosha kabisa kwa Guardiola kusahihisha makosa yake, ametamba kwamba leo hataingia tena Anfield na mbinu nyingine zaidi ya kuishambulia Liverpool mwanzo mwisho.

Guardiola alisema kwamba, mchezo wa leo hautafurahisha kama atawaambia vijana wake wajilinde na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Mpango huo kabambe wa Guardiola unatokana na takwimu ya Liverpool kupenda kufunga mabao katika dakika 45 za kwanza dhidi ya City, Reds wamefunga mabao 12 dhidi ya matatu ya kikosi cha mabingwa hao watetezi.

“Huwa sielewi kwanini ujilinde katika mechi kubwa kama hii. Timu yangu haitakaa nyuma na kujilinda muda wote,” alisema Guardiola.

“Kwanza niwaambie tu, soka la kujilinda linakera sana, halafu sikuitengeneza Man City iwe timu ya kujilinda. Huwa nawasihi wachezaji wangu wacheze soka lao, si kwenye viwanja vingine tu, hata Anfield.

“Na sio kwamba hatutalinda lango letu, ila hatuwezi kucheza na akili hiyo tu muda wote wa mchezo, kwa sababu tuna wachezaji ambao lazima waoneshe uwezo katika mechi kubwa,” aliongeza kocha huyo.

Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kuanza kwa mtanange huo, Guardiola ataingia Anfield na rekodi ya kupoteza michezo saba kati ya 14 aliyokutana na Jurgen Klopp.

Mchezo huo wa leo ni muhimu kwa pande zote mbili, ambazo hazijapoteza mechi ya Ligi Kuu England, zote zikiwa na rekodi ya kushinda mechi sita na kutoa sare moja kati ya saba walizocheza.

Ingawa kupoteza mechi si desturi ya Liverpool msimu huu, Reds hao watawakaribisha City bila kuwa na ushindi katika mechi tatu za mwisho walizocheza, ikiwamo sare dhidi ya Chelsea katika mchezo wa Ligi Kuu.

Aidha, City ndio vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, wakiipita Liverpool kwa tofauti ya mabao sita ya kufunga, lakini wakati huo huo bado wenyeji watakuwa na cha kujivunia leo.

Mpaka sasa City imekutana na timu zilizo na wastani wa kushikilia nafasi ya 14.7 katika msimamo, zikiwamo nne ambazo zinasuasua katika nafasi za kushuka daraja, wakati Liverpool tayari wameshazivaa timu kwa wastani wa nafasi ya 10.4.

Kikosi cha Liverpool kitaendelea kumkosa viungo wao, Chamberlain, anayeuguza jeraha la goti na Adam Lallana, lakini Naby Keita huenda akaonekana dimbani leo, licha ya kuumia mgongo dhidi ya Napoli.

Guardiola yeye alithibitisha kwamba kiungo wake, Kevin De Bruyne amepona goti na alishaanza mazoezi na wenzake, na huenda akacheza leo, lakini viungo wengine, Fabian Delph na Ilkay Gundogan hawatacheza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.