OKWI ATOA MKOSI LIGI KUU2

Apiga bao, Simba ikiiua A.Lyon 2-1

Dimba - - Mbele - NA SAADA SALIM

STRAIKA wa kimataifa wa Simba, Mganda Emmanuel na winga Shiza Kichuya wameondoa mkosi wa ukame wa mabao katika Ligi Kuu baada ya jana kila mmoja kutupia katika ushindi wa 2-1 timu hiyo iliyoupata mbele ya African Lyon, mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mara ya mwisho Okwi kufunga ilikuwa Mei 6, 2018 mwaka huu katika mchezo wa Simba dhidi ya Ndanda uliomalizika kwa wekundu hao kuondoka ushindi wa bao 1-0.

Kichuya naye katika michezo mitano ya Ligi Kuu aliyokwishaichezea Simba alikuwa hajacheka na nyavu huku mara ya mwisho kufunga ikiwa ni Februari mwaka huu 26 dhidi ya Mbao FC timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 5-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa Okwi ambaye ni mfungaji bora msimu uliopita bao hilo alilofunga dakika ya 47 limefungua rasmi akaunti yake kwani ikumbukwe tangu kuanza kwa msimu huu alikuwa hajatupia nyavuni.

Ushindi wa Simba jana ni wa nne katika mechi sita ambazo Simba imeshacheza ambao umeiwezesha kuchumpa hadi nafasi ya tatu katika msimamo Ligi hiyo na kuwapumilia kwa karibu vinara Mtibwa Sugar na Singida United.

Mtibwa Sugar wanaongoza Ligi hiyo wakiwa na pointi 17 wakifuatiwa na Singida United yenye alama 16 huku mabingwa hao watetezi wakifikisha pointi 14 kwa ushindi huo dhidi ya African Lyon.

Katika mchezo huo wa jana,Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kuliandama lango la Lyon kupitia kwa winga Shiza Kichuya na ambaye dakika ya nane ya mchezo alifanikiwa kuwanyanyua vitini mashabiki wa timu hiyo akiunganisha vyema krosi ya Shomari Kapombe na kujaza mpira wavuni.

Simba iliendeleza mashambulizi ya nguvu langoni mwa Lyon, dakika ya 11 nusura wapate bao la pili kama sio shuti hafifu alilopiga Okwi kudakwa na kipa Tonny Charlse.

Lyon walijibu mashambulizi ya Simba dakika ya 28 baada ya kupata nafasi ya wazi kufunga lakini Kassim Ndowe akaipoteza kizembe kwa kupiga shuti dhaifu likadakwa na kipa Aishi Manula.

Hadi mapumziko Simba walitoka kifua mbele kwa bao hilo moja.Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Lyon kutaka kusawazisha ambapo walifanikiwa kupata bao dakika ya 61 baada ya Awadh Juma kumchungulia Manula na kuamua kupiga shuti la mbali lililoingia moja kwa moja nyavuni.

Kocha wa Simba kwa mara kwanza jana alimtumia kiungo Haruna Niyonzima ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali.

Niyonzima ambaye ana dakika 450 akiwa nje ya uwanja baada ya kucheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Majimaji ya Songea na kufunga bao moja, aliingia dakika ya 77 akichukua nafasi ya Chama.

Huu ni ushindi wa pili kwa Simba bila Kocha Msaidizi wa timu hiyo Masoud Djuma. Ushindi wa kwanza ulikuwa ni ule wa Mwadui FC ambao Simba ilishinda mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja Kambarage Shinyanga.

Simba: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein √ęTshabalala, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Clatous Chama/ Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya/ Mohamed Ibrahim, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/ Said Ndemla.

African Lyon: Tonny Charles, Daud Mbweni, Baraka Jaffar, Augostino Samson, Emmanuel Simwanza, Said Mtikila, Awadh Juma, Ismail Adam, Kassim Ndowe, Victor da Coasta na Thabit Hamis.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.