Hamasa Taifa Stars iendelee kila kona

Dimba - - News -

WATANZANIA wanazidi kuonyesha hamasa kwa timu ya Taifa, wakati huu inapojiandaa kwa ajili ya mchezo wake wa michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya timu ya taifa ya Cape Verde. Amsha amsha ya Watanzania imeanza kuonekana tangu Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike, alipotangaza kikosi na inazidi kuendelea kadri siku zinavyozidi kwenda kufikia Oktoba 16, siku ambayo mchezo huo utapigwa. Tofauti na mechi nyingi za Stars zilizopita, wapenzi wa soka safari hii wanaonekana kukiamini kikosi cha timu hiyo tangu pale kilipocheza mechi ya kwanza dhidi ya timu ya taifa ya Uganda na kupata matokeo ya suluhu 0-0. Moja ya hamasa iliyopo miongoni mwa mashabiki wa soka kutoka kila kona ya Tanzania ni ahadi ya serikali kutoa ndege yake kwa ajili ya kupeleka mashabiki pamoja na wachezaji nchini humo kushuhudia mechi hiyo ya kimataifa. Sisi Dimba kwa nafasi kubwa kabisa tunaipoingeza Serikali kwa kukubali kuungana na mashabiki kwa kutoa usafiri huo, ambao licha ya kuwa na ahadi, lakini pia unawajenga wachezaji na mashabiki wake kisaikolojia na kujiona wana haki ya kupata ushindi kama zilivyo timu za mataifa mengine yaliyoendelea. Pamoja na hayo, lakini usafiri huo utakuwa wa haraka, ambao utasaidia wachezaji kutumia muda mfupi na hivyo kufika wakiwa na nguvu za kuikabili timu hiyo katika ardhi yake. Tunawatakia wachezaji wetu maandalizi mema, pia tunawahamasisha mashabiki wote wa soka hapa nchini kuhakikisha wanapata nafasi ya kusafiri na timu hiyo kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu nje ya uwanja ili kwa pamoja tulete ushindi Tanzania.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.