KUMBE MIKONO YA ALISSON BECKER NI HATARI KWENYE GITAA

Dimba - - Dimba Special -

TIMU ya Liverpool ilikamilisha usajili wa mlinda mlango wa AS Roma, Alisson Becker, ambaye aliweka rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi ulimwenguni kwa dau la pauni milioni 67. Lakini kwa muda wa wiki moja, klabu ya Chelsea ilivunja rekodi hiyo kwa kumsajili Kepa Arrizabalaga, kwa pauni milioni 71 kutoka Athletic Bilbao. Becker alivunja rekodi ya usajili iliyowekwa na kipa wa Manchester City, Ederson Moraes, kutoka Benfica msimu uliopita ya dau la pauni milioni 35. Usajili wa Becker katika kikosi cha Liverpool umekuja baada ya kipa aliyetolewa kwa mkopo Besiktas, Loris Karius, kuwa kwenye kiwango kibovu kilichopelekea kufanya makosa na kufungwa dhidi ya Real Madrid, ndani ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kipa mwingine, Simon Mignolet, akiwa katika kiwango kibovu tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu England na kuwekwa benchi na Karius. Inawezekana mashabiki wa Liverpool walikuwa katika wakati mgumu pindi timu hiyo ilipofungwa na Napoli kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa nchini Italia. Lakini haikuwa hivyo kwa wachezaji wawili wa Liverpool, Roberto Firmino na Becker, juzi waliosherehekea pamoja siku zao za kuzaliwa. Firmino na Becker wote ni raia wa Brazil, ambao wamezaliwa Oktoba 2, 1992. Kilichowashangaza wengi kwenye sherehe hiyo ni uwezo mkubwa wa kipa huyo wa Liverpool kupiga gitaa. MPIGA GITAA Upande wa pili wa kipa huyo amekuwa akipenda sana muziki, hasa kupiga gitaa ambalo alifundishwa wakati yupo mdogo katika shule ya muziki aliyosoma.

Hata akiwa mapumzikoni hupenda kupiga gitaa, ikiwa ni starehe yake nyingine ya kupenda muziki, huku akikumbukwa kufanya shoo ya muziki katika kipindi cha Danilo Gentili nchini Brazil.

ALIKUWA DHAIFU

Pamoja na mambo mengi yaliyokuwa kikwazo katika safari yake ya kucheza soka la ushindani, alishindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Internacional ya Brazil.

Becker alikuwa na tatizo la kukua lililopelekea mwili wake kuonekana dhaifu, huku akiwa na mwili mdogo zaidi uliopelekea kuwa chaguo la tatu katika kikosi cha vijana cha klabu yake.

Ilimpelekea kukata tamaa kiasi cha kutaka kuachana na soka, lakini subira na ushauri kutoka kwa watu wake wa karibu ulitoa matunda baada ya mwaka mmoja uliofuata aliongezeka inchi saba.

FAMILIA YA SOKA

Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wanaotokea katika familia za soka, hata kipa huyo mpya wa Liverpool aliyedaka kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na Brazil alikuwa hivyo.

Becker amefuata nyayo za kaka yake, Muriel, ambaye alikuwa kipa namba moja wa Internacional, huku akikumbukwa zaidi kuanza kazi hiyo katika timu yao ya mtaani iliyojulikana kwa jina la Novo Hamburgo.

Haikuwa ngumu kwa Becker kufuata nyayo hizo kutoka kwa kaka yake tangu akiwa na miaka mitano, aliyemfundisha tangu udogo wake hadi sasa.

Muriel hivi sasa anakipiga katika kikosi cha Belenenses ya Ureno, huku Becker akimtaja kuwa shujaa wake aliyemhamasisha katika kazi hiyo.

UPINZANI MKALI

Mara baada ya kusajiliwa na AS Roma kutoka Internacional ya Brazil alikutana na upinzani mkubwa katika kikosi hicho chenye maskani yake Roma, Italia.

Kwa muda wote alikuwa chaguo la pili nyuma ya Wojciech Szczesny, aliyekuwa namba moja, huku akifanikiwa kucheza michezo 10 ya Ligi ya Europa pekee katika msimu wake wa kwanza.

Ilimchukua mwaka mmoja Becker kusimama golini kama kipa namba moja wa AS Roma, baada ya Szczesny kutimkia Juventus, huku ikibainika alikuwa tayari kuondoka kama asingepata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

MTU WA FAMILIA

Kama ilivyo kwa wachezaji wengine wanaopenda kujichanganya na familia zao katika muda wao wa mapumziko, basi hata kwa kipa huyo ipo hivyo. Becker ana mke anayejulikana kwa jina la Natalia, huku wakibarikiwa kupata mtoto wa kike waliyempa jina la Helena. Becker alianza mahusiano na Natalia mwaka 2012, hadi pale walipofunga ndoa mwaka 2015, wakisubiri mwaka mmoja zaidi hadi pale walipopata mtoto wao wa pekee. Pamoja na safari mbalimbali za timu, Becker anatajwa kuwa mtu anayependa kutulia nyumbani na familia yake pindi anapokuwa mapumzikoni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.