TUNA KILA SABABU YA KWENDA CAMEROON

Dimba - - Nyuz Nyuz -

IMETOSHA miaka 38 kwa Taifa Stars kubaki jukwaani wakiwa watazamaji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon). Hakuna kaulimbiu nyingine tunayoweza kuibeba migongoni mwetu zaidi ya kusema imetosha tu.

Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 zilizopigwa nchini Nigeria ikiwa chini ya Kocha marehemu Joel Bendera. Taifa Stars ya Kocha Emmanuel Amunike ina kila sababu ya kutuondoa jukwaani na kutupeleka Cameroon kibabe.

Sioni nini cha kutufanya tusiandike historia mpya Afrika, ikiwa tuna kikosi kipana cha Stars chini ya kocha mwenye rekodi ya mataji.

Ukiacha maandalizi ya kiufundi ambayo Stars inaendelea kuyafanya kambini jijini Dar es Salaam, pengine huu ndo wakati muhimu kwetu kumlilia Mungu kwa maombi, iwe zamu yetu nasi kwenda Cameroon, ambako fainali hizo zitapigwa mwakani.

Stars iko kwenye kampeni ya kuwania kushinda mechi nne za kufa na kupona ili kukata tiketi ya Afcon. Kikosi cha timu hiyo kilicho kundi L na timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho hakuna kingine kilicho mbele yake zaidi kushinda mechi hizo ili kukwea pipa kwenda Younde, Cameroon.

Ni kazi nyepesi kwa Stars kufuzu fainali hizo tu kama wachezaji wa timu hiyo watatambua thamani ya jezi ya timu hiyo na kuipigania kwa machozi, jasho na damu.

Miongoni mwa sababu za Stars kukwama kwa miaka zaidi ya 30 kufuzu Fainali za Afrika, ukiacha maandalizi dunia, ni pamoja na wachezaji kukosa uzalendo wa kuipigania jezi ya timu hiyo.

Kazi kubwa iliyo mbele ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sasa mbali na kubeba jukumu la maandalizi, inatakiwa kuelekeza nguvu ya kuongeza msisimko wa mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu hiyo.

Msimamo wa kundi ambalo Stars imo unaonyesha baada ya kila timu kucheza mechi mbili nafasi ya kufuzu iko wazi kwa yeyote. Kwanini tusiende Cameroon wakati milango iko wazi kwetu pia.

Baada ya kila timu katika kundi hilo kucheza mechi mbili timu ya Uganda, 'The Cranes' inaongoza kwa pointi nne walizonazo. Lesotho inakamata nafasi ya pili kwa alama mbili walizovuna sawa na Tanzania.

Taifa Stars na Lesotho zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga, huku Cape Verde wakishika mkia kutokana na alama moja waliyonayo.

Hatima ya Stars kufuzu iko mikononi mwa mechi zake zilizosalia, huku kazi kubwa ikiwa ni kushinda walau michezo mitatu tu na kutafuta sare moja ili kumaliza katika kundi hilo nafasi ya kwanza au ya pili.

Kikosi cha Stars kipo kambini jijini Dar es Salaam kujiwinda na mechi ya kuchonga barabara kuelekea Younde dhidi ya Cape Verde, itakayopigwa Oktoba 12, mwaka huu, mjini Praia.

Stars italazimika kusafiri kilomita 6,875, sawa na maili 4,272, ukiwa ni mwendo wa saa 7 na sekunde 63 kwenda kufuata ushindi mbele ya Cape Verde, kabla ya siku tatu baadaye timu hizo kurudiana Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ikumbukwe Stars ilianza kampeni ya kufuzu fainali hizo Juni 10, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kwa kukipiga na Lesotho na kubanwa mbavu kwa sare ya bao 1-1, kabla ya kuitoa jasho The Cranes kwao na kupata suluhu.

Kikosi hicho kimesaliwa na mechi mbili za nyumbani ambazo ni dhidi ya Uganda na Cape Verde, lakini kimbembe zaidi ni kwenda kutafuta ushindi ugenini mbele ya Lesotho na Cape Verde.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.