ZAMOYONI MOGELA

Dimba - - Burudani Za Wasanii - MBWANA SAMATTA VS ZAMOYONI MOGELA NA MNAZI WA WANAZI

NYOTA ya straika wa Kitanzania anayekipiga nchini Ugiriki yani Mbwana Samatta, imezidi kung'ara na hivi sasa kila kona ya wapenda michezo mjadala ni juu yake.

Naona ndiyo sababu hata hapa kwenye kijiwe chetu jina lake likawa la kwanza kuletwa na mbishi wetu hatari, Goal Machine ambaye baada ya kuweka mezani hoja yake tu naye mzee mzima anayejiita Mnazi wa Wanazi, akaja na hoja yake kwamba licha ya umaarufu wa Samatta, lakini kamwe asingeweza kunusa uwezo wa mkongwe wa soka wa zamani, Zamoyoni Mogela.

Sisi wasikilizaji tunaweka mezani kisha na wewe uone mada zao kisha utakuwa na maamuzi yako kichwani, ubishi wao umeanza kwa maelezo haya: KILA jambo lina wakati wake, hili siwezi kukataa huwezi ukapenda jua la asubuhi na ukaliwezesha liendelee kukuburudisha hata utakapotimu usiku, hayo hayatakuwa mamlaka yako.

Nitoe la moyoni ambalo si la kufikiria au kuhadithiwa bali ni la kuona mwenyewe nikilishuhudia soka la Tanzania kwa umri wangu wote huu uliofikia uzeeni sasa.

Nimelazimika kumtaja bila hofu straika wa zamani wa timu za Taifa, Yanga na Simba, Zamoyoni Mogela.

Nimeanza kwa kutaja suala la nyakati kutokana na ukweli kwamba, hapo zamani wakati wachezaji wengi wazuri wanacheza soka, dunia ilikuwa imefungwa, mawasiliano hayakuwa kama hii leo, teknolojia ilikuwa chini au wakati mwingine tuseme haikuwa rafiki katika kutafuta maendeleo hasa kwa nchi changa.

Hiyo ndiyo sababu iliyochangia wachezaji wetu wengi wazuri waliopita tangu enzi ya akina Abdallah Kibadeni, Abdrahman Juma, Sunday Manara na wengine washindwe kwenda kucheza soka nje.

Hizo fursa hazikuwepo, lakini sikubaliani hata kidogo na mtu anayeropoka akisema eti wengi hawakufikia kiwango anachokionyesha Samatta hivi sasa.

Ukiacha wote lakini lazima nijithibitishie mtu ambaye naweza kubishana hata wiki nzima bila kulala ni Mogela au Golden Boy enzi hizo akiitwa kwa jina hilo.

Hakuwa tofauti kabisa na wachezaji waliokuwa waking'aa enzi hizo, lakini ule ufinyu wa teknolojia ya mawasiliano ndiyo maana wakamaliza soka lao katika nchi hizi zetu za Afrika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.