Tshabalala, Ajib wanashawishi kuja uwanjani

Dimba - - Burudani Za Wasanii -

VIWANGO vya wachezaji wawili, nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib, vinashawishi sana kushuhudia mpira ukiwa miguuni mwao katika mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Tshabalala alikuwa chachu ya ushindi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu dhidi ya African Lyon waliokubali kichapo cha mabao 2-1.

Kwa upande wake, Ajib aliibeba Yanga mgongoni mwake aliposhindilia msumari wa mwisho mbele ya Mbao FC katika ushindi wa 2-0 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa Simba mbele ya African Lyon ulikuwa ni wa sita kwa Tshabalala kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kati ya mechi saba ambazo Mnyama ameshuka dimbani tangu kuanza kwa ligi.

Idadi hiyo ya michezo inamfanya Tashabalala kucheza jumla ya dakika 540, huku miongoni mwa mechi alizoonesha ukomavu kuwasha taa ya kijani kurejea katika kiwango chake cha misimu miwili iliyopita, ilikuwa ni Septemba 30, mwaka huu dhidi ya Yanga.

Naam. Kuonekana bora maradufu katika mchezo huo unaojaza mashabiki wengi jukwaani hapo ndipo ‘credit’ kutoka benchi la ufundi inamfikia Tshabalala kuendelea kumwamini.

Wastani mzuri wa kupiga krosi sahihi unaonekana kurejea kwa nyota huyo mwenye umbo dogo akiwa na matumizi mazuri ya nguvu, baada ya kuyumba msimu miwili iliyopita kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Minong'ono ya awali kuwa Asante Kwasi ambaye alicheza mechi nyingi zaidi msimu uliopita kwamba alikuwa anampoteza wakati huu haitakuwa ajabu kugeukia upande wa Kwasi. Bi- nafsi ninachokiona kizito kwa Tshabalala ni kitambaa cha unahodha. Si mzuri sana katika nafasi hiyo ndani ya uwanja hasa katika mawasiliano ikiwamo inapotokea utata hana uharaka wa kumwona mwamuzi.

Mfano mzuri ni mchezo uliowakutanisha na Yanga, Emmanuel Okwi alikuwa ameongea na mwamuzi, Jonesia Rukya kuliko yeye mwenye mamlaka hayo, ingawa bado ana nafasi ya kujifunza kwa mkuu wake, John Bocco.

Ibrahim Ajib ‘Ibra Cadabra’ yeye Jumapili bao la pili la mtindo wa ‘acrobatic’ alilowafunga Mbao alitukumbusha alichokifanya Septemba 27, mwaka jana dhidi ya Ndanda Uwanja huo huo wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali na bao hilo ambalo huenda likaingia katika orodha ya mabao bora mwishoni mwa msimu, lakini pia ulikuwa ni mchezo wake wa pili msimu huu ndani ya mchezo mmoja kuingia kimiani na kutoa asisti.

Mchezo mwingine aliofanikiwa kufanya hivyo ilikuwa ni wiki kadhaa zilizopita dhidi ya Singida United akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 4-3, pasi mbili za mwisho zikitoka mguuni mwake.

Mfumo unaotumiwa na kocha Zahera Mwinyi wa 4-3-3 yeye akionekana kama kiungo mchezeshaji, unampa uhuru zaidi wa kuzunguka eneo kubwa la uwanja. Udhaifu wake ni kwenye kukaba huku jukumu hilo akiwaachia Feisal Salum Toto na Papy Kabamba Tshishimbi.

Lakini bado haitoshi kuwaona Tshabalala na Ajib kuwa katika kinyang'anyiro cha wachezaji waliofanya vizuri mwishoni mwa msimu isipokuwa ni fahari zaidi kuwaona wakivuka mipaka ya nchi.

Hicho ndicho kilichofanywa na kina Simon Msuva, Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusin), Rashid Mandawa, Hassan Kessy (Nkana, Zambia), Himid Mao (Petrojet, Misri), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Farid Mussa na Shaban Idd wote kutoka Tenerife, Hispania.

Lakini bado haitoshi kuwaona Tshabalala na Ajib kuwa katika kinyang'anyiro cha wachezaji waliofanya vizuri mwishoni mwa msimu isipokuwa ni fahari zaidi kuwaona wakivuka mipaka ya nchi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.