AMBOKILE KIROHO SAFI KUTUA YANGA

Dimba - - Mbele - NA SAADA SALIM

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba yule straika wa Mbeya City wanayemfukuzia kwa udi na uvumba, Eliud Ambokile, amekubali kiroho safi kujiunga na kikosi chao.

Ambokile, ambaye amekuwa akihusishwa sana kujiunga na Wanajangwani hao, amesema yeye ni mchezaji halali wa Mbeya City na kama Yanga wanamtaka waende wakazungumze na timu yake na yeye atakuwa tayari kuvaa jezi za kijani na njano.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Ambokile alisema licha ya kwamba taarifa hizo za kutakiwa na Yanga anazisikia mitaani, lakini hazimzuii yeye kukubali kujiunga na timu hiyo kongwe, kwani ndiyo moja ya malengo yake katika soka.

ìNiseme wazi kwamba taarifa hizo za kutakiwa na Yanga nazisikia tu kwenye vyombo vya habari, mimi hawajanifuata ili tuzungumze, ninachoweza kusema bado nina mkataba na Mbeya City, lakini kama watazungumza na kumalizana nao sitakuwa na pingamizi".

Yanga wanahusishwa kuifukuzia saini ya straika huyo kutokana na umahiri wake wa kucheka na nyavu ili akaungane na Heritier Makambo, kwenye safu ya ushambuliaji ya Wanajangwani hao.

Katika msimamo wa ufungaji, Ambokile ana mabao saba kileleni sawa na mfungaji bora wa msimu uliopita, Emmanuel Okwi wa Simba, kitu ambacho kinawapagawisha Yanga kutaka wamsajili kipindi cha dirisha dogo. Kama Yanga watafanikiwa kumsainisha straika huyo, watakuwa na safu kali ya ushambuliaji, kwani Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, alishaweka wazi kwamba kuna straika mwingine kutoka DR Congo amekubali kutua dirisha dogo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.