SIMBA MECHI 10 TU ZAAMUA USAJILI MPYA

Dimba - - Mbele - NA MWANDISHI WETU

MECHI 10 za Ligi Kuu Bara iliyocheza Simba na kufanikiwa kushinda saba, ikitoka sare 3 na kufungwa moja, inaonekana kumpa jeuri kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems na kuona kwamba suala la usajili mpya kwake siyo ishu muhimu.

Hiyo inatokana na kuwa na kikosi kipana ambacho anaamini kitaendelea kufanya vizuri katika michuano hiyo ya Ligi na pia ile ya kimataifa.

Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wanatarajia kuiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, itakayochezwa mwishoni mwa mwaka huu. Dimba Jumatano lilimtafuta Kocha huyo raia wa Ubelgiji likitaka kujua tathmini fupi ya kikosi chake na pia mipango yake ya usajili kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi na kimataifa, ambapo alisema jambo hilo kwa sasa si muhimu tena.

"Ukiangalia kikosi changu utakuta kila namba ina wachezaji zaidi ya mmoja, hivyo ninachotakiwa kufanya sasa ni kuwaweka sawa hawa nilionao ili waimarike zaidi," alisema.

Kocha huyo alisema, moja ya sababu kubwa ya kung'ang'ania wachezaji 30 aliokuwa nao katika kikosi chake ni kutokana na kuwa nao kwa muda mrefu na kuwafanya wazoeane na kucheza kitimu zaidi.

"Asilimia kubwa ya wachezaji waliomo katika kikosi changu ni wale tulioanza nao na kufanya nao ziara ya mafunzo nchini Uturuki na ndio hawa wanaoendelea na Ligi, hivyo kuwaongezea wachezaji wageni itaweza kuwachanganya hapo baadaye."

Kutokana na uamuzi huo, inaonyesha kikosi hicho kitaendelea kuwa na wachezaji wake 10 wa kigeni ambao ni pamoja na staika anayeongoza kwa mabao, Mganda Emmanuel Okwi, Pascal Wawa, James Kotei, Harua Niyonzima, Meddie Kagere, Nicholaus Gyan, Jjuuko Murshid, Clatous Chama.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.