Nuhu anayeitengeneza safina ya maangamizi ya Borrusia Dortmund

Dimba - - NEWS -

YUKO wapi aliyewahi kusema tabasamu linaficha vitu vingi? Ni ngumu kujua kiasi gani cha maumivu mtu amekibeba moyoni, wakati mwingine mioyo yetu huficha siri ambazo kwa macho huzioni.

Kwa kiasi fulani huwa ni hisia ambazo ni ngumu kuelezeka kwa urahisi, iwe huzuni au furaha, hufika kipindi vyote huwa havielezeki kiurahisi zaidi ya kuona matendo ya mtu husika.

Hakuna wakati uliokuwa mgumu kwa mashabiki wa Borussia Dortmund kama kumwona, Jurgen Klopp, akipunga mkono wa kwaheri ndani ya timu hiyo.

Kama ni ndoto waliomba iishe mapema, inawezekana walikuwa kwenye wakati mgumu kiasi cha kuamini dunia yote ipo kwenye mabega yao.

Kwanini Klopp? Hakuna jibu lingine zaidi ya kusema alikuwa mwanadamu pekee aliyeitengeneza pepo ya Borussia Dortmund na kuifanya kuwa sehemu ya faraja kwao na chungu kwa wengine.

Kwa kipindi kirefu Klopp aliishi kama mfalme ndani ya ngome ya kikosi hicho, kila shabiki aliimba jina lake, hakika aliingia kwenye mioyo ya mashabiki hao.

Katika kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni ni Borussia Dortmund ya Klopp iliyoweza kuvunja utawala wa Bayern Munich, walitwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga mara mbili mfululizo, DFB Cup na Ngao ya Jamii.

Lakini kwa kipindi chote hicho aliifanya Bayern Munich kutambua uwepo wa Borussia Dortmund kama mpinzani mkubwa katika mafanikio yao kwa kuwania mataji.

Kuondoka kwa baadhi ya wachezaji nyota kulifanya timu hiyo kuanza kubomoka taratibu, pia, hata mkono wa kwaheri wa Klopp ulizidi kuwamwaga machozi mashabiki wa klabu hiyo nchini Ujerumani.

Kuna shabiki mmoja wa Borussia Dortmund anaamini kuwa yale mambo anayoyafanya Klopp ndani ya kikosi cha Liverpool, ilibidi ayafanye Signal Iduna Park.

Inaonyesha kwa kiasi gani mashabiki wa Borussia Dortmund waliamini Klopp ndiye Sir Alex Ferguson wao kwa kukaa ndani ya timu hiyo kwa muda mrefu na kuendelea kufurahia matunda yao.

Haikuwa hivyo tena, Waswahili huwa wanasema safari moja huanzisha nyingine, kuondoka kwa Klopp kulifungua milango kwa makocha wengine kuandika historia zao ndani ya Borussia Dortmund.

Thomas Tuchel, ni mmoja wa makocha walioingia baada ya kuondoka kwa Klopp, alijaribu kufanya kila kitu kuirudisha timu hiyo katika kilele cha ubora wake, lakini ilikuwa ngumu sana kwake.

Kila alichokifanya kilishindwa kufanyika alivyokihitaji na mwisho wa siku aliondoka ndani ya kikosi hicho.

Borussia Dortmund walirusha sarafu ya bahati kwa kocha wa zamani wa Ajax, Peter Bosz, kwa kifupi tunaweza kusema kamari waliyoicheza kwa kocha huyo ilishindwa kulipa kile walichokiamini.

Bosz hakudumu ndani ya Signal Iduna Park, yaani wasifu wake ulikuwa mfupi sababu aliingia Julai na kuondoka ndani ya kikosi hicho Desemba.

Hawakuchoka walihamishia imani zao kwa kocha kutoka Austria, Peter Stoger, ambaye alifanya kazi kubwa na kuirudisha timu hiyo katika ‘top four’ na kuwafanya kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Hata Stoger hakumaliza safari yake vizuri ndani ya Borussia Dortmund na kupelekewa kupoteza kibarua chake mwishoni mwa msimu uliopita.

Naamini tangu kuanza kwa msimu huu utakuwa umeiangalia na kuifuatilia timu hiyo kwa kiasi kikubwa na kushangazwa na kasi kubwa waliyoanza nayo.

Borussia Dortmund wapo kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Ujerumani, tena hawajafungwa mchezo wowote kati ya tisa waliyocheza mpaka hivi sasa.

Wanacheza mpira mzuri, wanafunga mabao ya kutosha lakini cha kushangaza imekuwa timu ambayo inaogopeka sana tangu kuanza kwa msimu huu.

Kila kitu kibaya kimebadilika kwao, kutoka kumaliza nafasi ya nne msimu uliopita mpaka kuongoza ligi msimu huu ni maendeleo makubwa sana kwao.

Mambo yanaonekana kuwaendea vizuri, kwa muda mfupi wamefuta utawala wa Bayern Munich ambao wapo kwenye shinikizo kubwa la kumfukuza kocha wao, Nico Kovac.

Safari ya Ligi Kuu ni ndefu sababu ya kuwa na michezo 34 kwa Bundesliga ambayo ina timu 18 zinazoshiriki, kwa maana hiyo chochote kinaweza kutokea huko mbele lakini kwa dalili walizoonyesha mwanzoni huwezi kukataa kuwa wanaweza kutwaa ubingwa msimu huu.

Nyuma ya kila kitu kilichobora hivi sasa kwa Borussia Dortmund amesimama mzee mmoja mwenye miaka 61, anaitwa Lucien Favre, ni moyo wa timu hiyo katika mafanikio hayo yanayoonekana.

Favre ni kocha mzoefu wa soka la Ulaya, anasifika kwa kutengeneza timu kama alivyoweza kuifanya Nice kuwa hatari katika Ligi Kuu Ufaransa na kuirudisha kwenye Ligi ya Mabingwa huku akiwa na straika mtukutu, Mario Balotelli. Hapo alifanikiwa.

Historia yake kama ingekuwa nchini England anafanana na Sam Allardyce maarufu kama ‘Big Sam’ ambaye anasifika kwa kupandisha timu daraja au kuzifanya kuwa bora na kusalia Ligi Kuu.

Favre ni raia wa Switzerland, hajulikani sana labda kuifanya Borussia Dortmund kuwa katika kilele cha ubora inaweza kumfanya kujulikana zaidi kwenye dunia ya soka.

Usajili wake alioufanya msimu huu kwa wachezaji kama Axel Witsel, Jadon Sancho, Abdo Diallo, Thomas Delaney, Marius Wolf na Paco Alcacer, kumeleta mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho.

Mikono ya Favre imefanikiwa kwa muda mfupi kuijenga Borussia Dortmund ambayo ilikuwa kwenye ndoto za mashabiki wa kikosi hicho wakati wa Klopp kabla ajajiunga na Liverpool.

Favre ni shujaa na moyo wa timu hiyo, kila linalotokea hivi sasa limepitia kwake ikiwa alishatuonyesha huko nyuma yeye ni kocha wa aina gani.

Na AYOUB HINJO Email: hinjo38@gmail.com

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.