Katika mabonde na milima tangu 1975

Dimba - - NEWS -

HUWEZI kuzungumzia bendi zilizowahi kutamba katika tasnia ya muziki wa dansi nchini ukaiacha bendi ya Bima Lee.

Awali ilijulikana kama Bima Jaz Band, kwenye miaka ya 1975 wakati huo ikianzishwa na wanamuziki wenye uwezo mkubwa na kuvamia anga ya muziki wa nguvu zote.

Ilikuwa katika miaka hiyo Bima hiyo ilipokuja na nyimbo kama Radhi ya Wazee, Sheri Rarifa na nyingine kadhaa.

Wakati huo licha ya bendi kuwa na wanamuziki wakubwa kama Patrick Kapama, Willfred Bon, Abdala Mbossanga na Kassim Mbossanga, lakini mtunzi aliyetegemewa zaidi ambaye pia aliikuwa ni ni marehemu Cosmson Mkomwa.

Huyu atakumbukwa sana kwa uwezo wake wa kupuliza saxafoni na pia kuimba akishiriki katika makundi kama vile Vijana Jazz, Orchestra Marquiz Du Zaire, Bima na pia alikuwa mwanachama katika bendi ya Cobash iliyokuwa pia na wanamuziki, Shaaban Yohana Wanted, Roy Mashekanano na Comson.

Maana ya Cobash ni Comson Bashekanano na Shaaban, ambao walirekodi kwa mtindo wa Zing zong nyimbo kama Maneno ni sumu na nyingine kadhaa.

Tuondoke huko kwa Cobash turudi Bima, mwaka 1976 kundi hili liliwahi kutoa nyimbo ambazo hata wenyewe wanakubali kwamba hazikufanya vizuri kutokana na kutokukubalika sana redioni lakini pia hazikupendwa sana na mashabiki.

Nyimbo hizo zilirekodiwa Machi 24, 1976 ambazo ni Siasa ni Kilimo uliotungwa na Abdalah Mbosanga, Ukombozi wa Afrika alioutunga Comson, Nick uliotungwa na mwimbaji chipukizi enzi hizo, Said Cats na wimbo ulioimbwa katika lugha ya Kihaya uitwao Omgonzigwa.

Lakini hatimaye kundi hilo likaingia na gia kubwa miaka miwili baadaye yaani 1978 na kurekodi kazi za hatari ukiwemo Uzuri wa Sofie ambao ulitosha kumsifia mwanamke mwenye macho ya gololi na mashavu ya kumimina.

Kuanzia hapo Bima Lee ikafanya mabadiliko madogo katika kikosi chake kama vile kumpata mpiga kinanda hatari enzi hizo, Kassim Magati, huku waimbaji akina Roy Bashekanako, Jumbe Batamwanya waliikamata vizuri staili yao ya Bima Lee.

Hili neno Lee lilitokana na kuhusudiwa kwa mavazi ya kampuni hiyo iliyokuwa inatangaza suruali za jinzi iliyoasisiwa tangu mwaka 1889 chini ya umiliki wa Henry David Lee.

Mpiga karate maarufu raia wa China, Lee Jun-fan, maarufu kama Bruce Lee, naye akalikuza na kulipa umaarufu sana jina la Lee.

Mwamba huyu alizaliwa Novemba 27, 1940, nchini China na kisha akafariki Julai 20, 1973.

Tuachane na Brice Lee, pale Bima mambo yakazidi kunoga baada ya kurekodi nyimbo Robi, Asia, Usilale na nyingine kadhaa.

Lakini shirika la Bima la taifa lililokuwa likimiliki bendi hiyo kwa hakika lilikuwa na nia ya dhati ya kuiendesha bendi hiyo kwa mafanikio.

Baada ya kukaa na wanamuziki walewale kwa kipindi fulani, waliona ipo haja ya kuongeza nguvu katika kundi hilo ili kuongeza mashabiki na kuinua aina ya muziki wake.

Ndipo Januri mwaka 1984 ilipoamua kuvunja benki na kusajili wanamuziki wengine wakali na waliokuwa na majina makubwa katika tasnia ya muziki nchini.

Hatiamaye majina ya Abdalah Gama, Joseph Mulenga na Suleyman Mwanyiro, waliokuwa nguzo ya bendi ya Mlimani Park walitangazwa kujiunga na bendi ya Bima Lee.

Hawa walikuwa mapacha wa upigaji wa magitaa, Mulenga solo, Mwanyiro besi na Gama ridhim gitaa.

Kadhalika waimbaji wawili walichukuliwa toka bendi ya Vijana ambao ni Athumani Momba na Jerry Nashon maarufu kama Dudumizi.

Kana kwamba haitoshi, wakapeleka tena msiba katika bendi ya Mlimani Park kwa kumnyakuwa mwimbaji, Shaaban Dede.

Hawakuchukua muda mrefu kuingia katika studio na kurekodi kazi zao za kwanza.

Machi 2, 1984 wanaume hawa wakaingia kazini na kurekodi nyimbo sita, zilizotokea kumgusa kila mpenzi wa muziki na kuifanya tasnia ya muziki enzi hizo kuongeza ushindani wa hali ya juu.

Gama, marehemu Muhidin Gurumo, Shaaban Lendi na wanamuziki wengi waliwahi kukiri kwamba mwaka huo ulikuwa na ushindani wa hali ya juu.

Hiyo ilitokana na makundi makubwa kipindi hicho kama OSS ikiwa chini ya Ndalla Kasheba, Tuncut Alimas, Juwata Jazz na Mlimani Park, kujiandaa vilivyo ili kupambana na ushindani wa kimuziki.

Nyimbo zilizorekodiwa tarehe hiyo niliyotaja hapo juu ni Fungua macho aliotunga Gama, Mzigo nimeutua utunzi wake Mulenga na Selina alioutunga Mwanyiro.

Selina ndio wimbo pekee kati ya hizi za mwanzoni alizoshiriki kuimba Dede, nyingine zilifanyiwa mazoezi kabla mipango ya kumchukua yeye haijakamilika.

Nyingine tatu alizitunga Mulenga ambao ni Fanya kazi, Moyo wangu na Picha yako.

Bendi hiyo iliyokuwa ikifanya maonyesho yake mengi katika Ukumbi wa Mbwisi Bar uliopo Manzese na Omax Bar Keko pia ilikuwa na wanamuziki wengine ambao walikuwa wenyeji katika kundi hilo.

Miongoni mwao ni Joseph Nzengula, aliyekuwa pia akipiga solo, Duncun Ndumbaro, aliyekuwa akipiga ridhim, Hamisi Sama na Salum Urembo, hawa walikuwa wakipiga besi.

Wapulizaji matarumbeta walikuwa wawili, Juma Masalawa na Lazaro Remmy, lakini saxafoni alikuwepo gwiji Shaaban Lendi, ambaye hadi sasa yupo na bendi ya Mlimani park.

Said Mharami, alikuwa akipiga tumba na Athumani Manicho, alikuwa akipapasa dram.

Ukiacha akina Dede waimbaji waliokuwepo ni pamoja na Roy Bashekanako, Belesa Kakere, Jumbe Batamwanya, walioshirikiana na kuibua vibao hivyo vya awali.

Kundi hilo baadaye liliendelea kubadilika na kubadili sura za wanamuziki wakaingia wengi hadi pale shirika lilipoamua kuivunja bendi na kumaliza historia ya bendi hiyo.

JIMMY CHIKA jimmchikah@yahoo.com 0712 328 223

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.