Si kila anayesema anakupenda anamaanisha...

Dimba - - NEWS -

LEO tunajadili somo muhimu sana kwa ajili ya wanandoa na ambao wanatarajia kuingia kwenye ndoa. Kabla ya kwenda mbali zaidi, hebu tujiulize, unaposema; nakupenda, unamaanisha nini?

Tulia kwa muda, tafakari...mpenzi wako anapokuambia anakupenda, unafikiri nini zaidi kichwani mwako? Marafiki hapo ndipo kwenye msingi mzima wa mada yetu. Wengi huishia kufikiri kirahisi rahisi tu, kuwa anampenda fulani au mwezi wake anampenda!

Je, umewahi kujiuliza, unampenda mpenzi wako kwa kiwango gani? Je, yeye anakupenda kwa kiasi gani? Upendo wake unamaanisha nini hasa? Upendo wako kwake una maana gani? Ni pendo la ndani kweli au tamaa za mwili?

Unaweza kujiuliza, inawezekana vipi, ukampenda mtu hadi mkafikia kuingia kwenye ndoa, bado ikawa ni tamaa ya ngono tu? Hapa namaanisha kuwa yawezekana vipi, mpendane halafu muingie ndani maelewano yaondoke?

Heshima itoweke? Upendo utoweke? Inawezakana vipi? Wengi wanajiuliza: “Tumependana na mume wangu kwa miaka mingi, tumeingia kwenye ndoa na tumeishi humo kwa siku nyingi lakini kwanini leo hii nimuone amebadilika?”

Wasomaji wengi wananiuliza maswali yanayofanana na hayo (hasa wanawake). Ngoja nikupe kisa cha msomaji mmoja mwanamke, kisha tuingie kwa undani zaidi katika mada yetu.

KUTOKA KWA MSOMAJI:

Mimi nipo kwenye ndoa kwa miaka sita sasa, mimi na mume wangu tumejaliwa kupata watoto wawili, wa kike na wa kiume. Miaka mitatu ya mwanzo tuliishi kwa amani na upendo, nilipojifungua mtoto wa pili ndipo mabadiliko yakaanza.

Nimejikuta sina msisimko kabisa na mume wangu. Yaani nikimwangalia namwona wa kawaida tu, hanishawishi kwa chochote. Tatizo ni nini? Naomba ushauri wako.

TUNAJIFUNZA NINI?

Naamini wanawake wengi wana tatizo kama la msomaji wetu huyo. Si wanawake tu, hata wanaume nao wapo ambao hawana mvuto tena kwa wake zao. Wanaona wa kawaida kabisa, hakuna msisimko wala ushawishi.

Wanatazamana kama magogo tu, maana hakuna jambo jipya linaloonekana mbele ya uso wa macho yao. Ni kweli, tatizo hili lipo, tena linatafuna sana ndoa nyingi. Swali la msingi hapa, kama msomaji huyo anakiri alimpenda mumewe kwa dhati, wakafunga ndoa, iweje leo abadilike?

Ikiwa alikubali kwa hiari yake kuunganishwa na mumewe, tena hadi wamefikia hatua wamezaa, mapenzi yamekwenda wapi? Hapo ndipo kwenye somo lenyewe ambalo bila shaka ndiyo itakuwa tiba ya wote wanaosumbuliwa na tatizo hili.

KUPENDA NA KUPENDWA

Kitu cha msingi ambacho unatakiwa kujifunza hapa ni kwamba, pendo la dhati huishi ndani. Penzi huwa haliishi, halina muda maalumu wa kuishi ndani ya mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kama ulimpenda miaka 20 iliyopita kwa dhati ya moyo wako, basi leo huwezi kumchukia.

Upendo ukishaingia ndani ya moyo wa mtu hubaki humo milele, ila kuna mambo madogo madogo au pengine yanaweza kuwa makubwa, yanayoweza kusababisha kuuahirisha upendo kwa muda.

Nasema kuuahirisha kwa sababu hauwezi kuondoka. Rafiki zangu, ujue wazi kuwa, hadi mwenzi wako ameamua kuungana na wewe katika ndoa, si bahati mbaya. Hajabahatisha, bali amekuchagua kutoka kwa wengi.

Kama ndivyo, kwanini penzi liondoke ghafla? Haiwezekani. Kwa maana hiyo, sasa ni wazi kuwa penzi huharibiwa na sisi wenyewe. Kuna mambo ambayo yakifanyika hupunguza nguvu ya mapenzi na mwisho wake kusababisha matatizo kama nilivyoeleza hapo juu.

KWANZA JITAMBUE

Lazima ujitambue, ujue nafasi yako kwa mwenzako kisha uhakikishe unasimama sawasawa. Usipojitambua hutaona thamani ya mapenzi, hutaona umuhimu wako kwenye ndoa. Muunganiko wenu hautakuwa wa maana kama hutatambua thamani yako.

Lazima mwanamke asimame katika nafasi yake na mwanaume naye asimamie nafasi yake. Kuna baadhi ya watu wakishaingia kwenye ndoa wanaona kila kitu kimeshaisha. Hawaoni umuhimu wa kufikiria kuwa bora zaidi kwenye ndoa.

Ndugu zangu, nyumba inajengwa tena inajengwa kwa umakini wa hali ya juu sana. Huwezi kumwona mwenzako mpya kama wewe mwenyewe hujaonyesha upya katika mambo yako. Mvute mwenzi wako ili akuone kweli unahitaji kuwa mpya, hapo utatengeneza nafasi kwake kubadilika kwenye nyendo zake.

Marafiki, wiki ijayo tutaendelea na somo letu, usikose!

Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kwa njia ya simu kupitia group letu la WhatsApp? Wasiliana nami kwa simu 0718 400 146, nitakuunga. Njoo inbox ya WhasApp tafadhali. Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano. Ameandikia vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.