WALIWAKUNG’UTA SIGARA 1992

Dimba - - NEWS - NA HENRY PAUL IONGONI

Mmwa matukio yaliyowahi kufanywa na timu au wachezaji wa enzi hizo, moja ni lile lililofanywa na klabu ya Yanga yenye maskani yake makuu mtaa wa Jangwani na Twiga baada ya kuifunga timu ya Sigara mabao 2-1 yaliyopatikana kwa mikwaju ya penalti ‘matuta’.

Mchezo huo ambao ulikuwa ni mkali na wa kusisimua kwa muda wote wa dakika 90, ulikuwa ni wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Mei 9, 1992.

Sigara ambayo ilicheza ikiwa na wachezaji 10 kwa dakika 27 za mwisho ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 17 ya kipindi cha kwanza, lakini bao hilo lilirudishwa na Yanga kabla ya mapumziko kwa bao la penalti ‘tuta’.

Sigara ilipata bao lake kutokana na mpira safi wa kichwa uliopigwa na Julius Mwakatika kufuatia kona ilichongwa na Juma Shomari.

Baada ya bao hilo mchezo ulichezwa kwa nguvu huku kukiwa na rafu za hapa na pale kutoka kila upande. Katika dakika ya 26 na 27 kiungo Stephen Mussa na Issa Athumani walijaribu kupiga mashuti makali ambayo yalipaa juu ya lango.

Yanga ilipata bao la kusawazisha katika dakika ya 33 baada ya beki Abubakar Kombo kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi Hamisi Mwenda kutoka Dodoma akaamuru ipigwe penalti. Stephen Mussa alifunga penalti hiyo.

Baada ya bao hilo Sigara walilisakama lango la Yanga kwa mashambulizi makali na katika dakika ya 40, Abunu Issa, alipiga kiki kali kutoka kama mita 35 ambalo lilidakwa na kipa Stephen Nemes.

Dakika moja kabla ya mapumziko kiungo Method Mogela wa Yanga alifanya kazi nzuri alipookoa mpira uliokuwa unaelekea wavuni na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda. Mogela aliokoa hatari hiyo baada ya wachezaji wa Sigara kugongeana vizuri na Joseph Machela kutoa pasi kwa Machael Burton, huku akiwa na kipa Nemes amevutika alipiga kiki ya juu iliyokuwa inaelekea kutinga wavuni, lakini Mogela akiwa hajulikani alitoka wapi akaokoa mpira huo. Yanga ilianza kipindi cha pili kwa kishindo na katika dakika ya 51, Hamisi Gaga, alipiga kichwa kilichotoka nje kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Abubakar Salum.

Katika dakaika ya 61 wachezaji wa Sigara walimzonga mwamuzi Mwenda wakidai kuwa Method hakuchezewa vibaya. Katika kumzonga huko Mwenda aliwapa kadi za njano wachezaji watano wa timu hiyo. Hata hivyo, baadaye wachezaji wa Sigara walikubali mpira huo wa adhabu upigwe.

Katika dakika ya 72 Sigara nusura wapate bao kutokana na Burton kupiga kiki kali iliyogonga mti wa goli na mpira kurejea uwanjani na kudakwa na kipa Nemes.

Katika dakika ya 72, Yanga walipata bao la pili na la ushindi kutokana na mpira wa penalti baada ya beki Iddi Cheche kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Mwenda kuamuru ipigwe penalti. Gaga alifunga penalti hiyo.

Hivyo hada dakika 90 za mchezo zinamalizika Yanga walitoka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakiwa vifua mbele baada ya kuwafunga Sigara mabao 2-1 yaliyofungwa kwa ‘matuta’.

Kikosi cha Yanga kiliwakilishwa na Stephen Nemes, David Mwakalebela, Joseph Lazaro, Godwin Aswile, Said Zimbwe (marehemu), Method Mogela (marehemu), Abubakar Salum ‘Sure Boy’/Thomas Kipese, Hamisi Gaga ‘Gagarino’ (marehemu), Issa Athumani (marehemu)/Stephen Mussa (marehemu), Justine Mtekere (marehemu) na Kenneth Mkapa.

Sigara iliwakilishwa na Mohamed Nyalusi, Abubakar Kombo, Amir Shomari, Mustapha Hoza, Iddi Cheche, Aziz Nyoni, Ladislaus Shawa (marehemu), Iddi Msigara, Abunu Issa, Julius Mwakatika, Michael Burton na Hassan Martin/Joseph Machela.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.