KAGERE ANOGESHA UCHAGUZI SIMBA

Apiga bao 2 Simba ikiiua JKT, leo kama wote katika uchaguzi

Dimba - - MBELE - OSCAR ASENGA NA TIMA SIKILO, TANGA

KAMA ulidhani dozi za Simba zinaishia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, utakuwa umekosea na hilo wamelithibitisha jana wakiwafunga JKT Tanzania mabao 2-0, wakiwa uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani jijini Tanga.

Shujaa katika mchezo huo alikuwa straika matata, Meddie Kagere, waliyemsajili kutoka Gor Mahia ya Kenya akifunga mabao yote mawili kutokana na kazi nzuri ya Emmanuel Okwi.

Simba waliingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kufunga mabao mengi katika mechi mbili zilizotangulia ambapo waliiadhibu Alliance mabao 5-1 na baadaye kuipapasa Ruvu Shooting mabao 5-0 mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa.

Ushindi huo wa jana ni kama vile umenogesha uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo eneo la Ocean Road Posta jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwapata viongozi wapya baada ya waliopo madarakani muda wao kumalizika.

Simba walianza kuonyesha dalili za kutafuta ushindi mapema katika sekunde ya 40 walipofanya shambulizi kali, lakini shuti la Okwi likamgonga John Bocco na kutoka nje.

Dakika ya sita ya mchezo huo, JKT Tanzania walijibu mapigo kwa kufanya shambulizi la hatari lakini shuti kali lililopigwa kutoka winga ya kulia lilipanguliwa na kipa Aishi Manula na wakati mpira ukitaka kuingia wavuni James Kotei akatumia juhudi na kuuokoa.

Furaha kwa mashabiki wa Simba ilianza katika dakika ya 11 baada ya Kagere kupachika bao wavuni akiunganisha mpira wa Okwi ambaye alikuwa akijaribu kuwachambua walinzi wa JKT Tanzania lakini ukaokolewa na mpira kumkuta Kagere aliyefumua shuti kali kwa guu lake la kulia lililomshinda kipa wa JKT Tanzania.

Nusura Simba wajipatie bao la pili dakika ya 14, lakini mpira uliopigwa na Bocco kutokana na faulo, ulishindwa kujaa wavuni na dakika mbili baadaye JKT Tanzania nao walifanya shambulizi kali lakini shuti kali la Aziz Gilla liligonga mwamba na kurudi uwanjani na kuokolewa na mabeki wa Simba.

Kagere alizidi kupeleka furaha kwa mashabiki wa Simba, baada ya kufunga bao la pili katika dakika ya 38 akiunganisha mpira wa Okwi alioupiga kwa njia ya faulo ukagonga mwamba wa juu na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao hayo 2-0.

Kama Kagere angekuwa makini angefunga hat-trick kwani katika dakika ya 46 kipindi cha pili, Bocco alipiga shuti likagonga mwamba na kurejea uwanjani na straika huyo akashindwa kuuwahi mpira ambao uliokolewa na mabeki wa JKT Tanzania.

Kipindi hicho cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya kuwatoa baadhi ya wachezaji na kuingiza wengine lakini matokeo yaliendelea kubakia 2-0 mpaka dakika 90 zilipomalizika.

Katika tukio jingine, straika wa JKT Tanzania, Ally Shiboli, alilimwa kadi nyekundu kwa kile kinachodaiwa kumtolea lugha chafu mwamuzi wa mchezo huo ikiwemo kumzaba kofi.

Kikosi cha JKT Tanzania kiliwakilishwa na Abdulrahmani Mohamed, Aanuary Kilemile/Alli Bilab, Salim Gila, Frank Nchimbi, Rahim Juma, Madenge Ramadhani, Mwinyi Kazimoto, Kelvin Nashon/ Nassor Kapama, Hassan Materema, Abdulrahaman Mussa/Ally Shiboli na Edward Songo.

Simba walikuwa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga/Shiza Kichuya, Meddie Kagere/Mzamiru Yassin, John Bocco na Emmanuel Okwi/Said Ndemla.

Matokeo ya michezo mingine ya Ligi Kuu Bara jana ni kwamba, wazee wa ‘kupapasa’, Ruvu Shooting, walijikuta wakipapaswa wao baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, Alliance wakizinduka usingizini na kushinda bao 1-0 dhidi ya Singida United huku Biashara United wakilazimishwa sare ya kutofungana na Mbao FC.

Straika Meddie Kagere wa Simba akishangilia kwa staili ya aina yake

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.