MANJI ATULIZA MZUKA YANGA

Dimba - - MBELE - NA CLARA ALPHONCE

SIKU mbili baada ya kauli ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhitimisha filamu ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, kurejea katika klabu hiyo hali ya taharuki iliibuka miongoni mwa wapenzi wa klabu hiyo.

BMT kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Alex Nkeyenge, ilitoa msimamo wa mwenyekiti huyo kwamba ameamua kuachana na uongozi katika klabu hiyo aliyoiongoza kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba.

Wanachama kwa kipindi chote tangu ulipofanyika mkutano Juni 11, mwaka huu, ambao ulipitisha maamuzi ya kutoikubali barua yake ya kujiuzulu na kuendelea kumtambua kama mwenyekiti wa klabu hiyo, walikuwa na imani kwamba siku na saa yoyote kiongozi huyo angerejea na kuendelea kutoa mchango wake katika klabu.

Hivi karibuni kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alikaririwa akieleza matarajio yake ya kufanya usajili wa kutisha katika kipindi cha dirisha dogo baada ya kupata taarifa ya kurejea mfanyabiashara huyo.

"Nina imani Manji atarudi na tutafanya usajili mzuri kwa ajili ya ligi ya ndani na pia mechi za kimataifa," alisema Zahera.

Tayari Mkongomani huyo ameweka wazi sehemu ambazo anahitaji kufanyia marekebisho na baadhi ya wachezaji wameshaanza nao mazungumzo.

Lakini juzi baada ya BMT kulipua bomu hilo ndipo sintofahamu ilipozidi kuwavuruga Wanayanga ambao timu yao ipo katika mbio za kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo leo wanajitupa uwanjani kukipiga na timu ya Ndanda FC.

Lakini jana kauli ya Mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo, Bakili Makele, kwa kiasi kikubwa imerudisha matumaini kwa Wanayanga, wakiamini kwamba kiongozi wao huyo aliyejiweka pembeni kwa muda wa mwaka mmoja huenda akarejea tena kuisaidia timu yake.

Licha ya Makele kiongozi mwingine aliyeongeza pumzi ya matumaini kwa Wanayanga ni msemaji wao, Dismas Ten, ambaye aliwataka wana Yanga kuwa watulivu na kusubiri uchaguzi mkuu kama kuna jingine basi taarifa rasmi itatoka katika klabu.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa nyingine zinadai kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Yanga, George Mkuchika, amepigilia msumari wa mwisho baada ya kusema kuwa uchaguzi Yanga hauepukiki.

Pia Mkuchika alisisitiza kuwa lazima wafanye uchaguzi kujaza nafasi ambazo zimetangazwa na Serikali kupitia Baraza la Michezo Taifa (BMT).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.