Wanasimba jahazi lipo mikononi mwenu

Dimba - - NEWS -

WANACHAMA wa klabu ya Simba leo ndiyo siku yao muhimu ya kupata uongozi wa wajumbe watakaowawakilisha wenzao katika Bodi ya Wakurugenzi. Uchaguzi huo upande wa wajumbe wanaume kunatarajiwa kuwa na mvutano mkubwa kutokana na idadi yake kufikia 15 huku wakitakiwa watano kujaza nafasi zinazohitajika. Kwa ujumla uchaguzi huo utakuwa na masanduku matatu, moja likiwa ni kwa ajili ya kura za mwenyekiti, jingine la wajumbe wanaume na la mwisho ni wanawake. Tumejaribu kufafanua hili ili kuwapa ufahamu baadhi ya wajumbe ambao wanaweza kujichanganya na hivyo kushindwa kuitumia vizuri haki yao ya msingi. Lakini baada ya maelekezo hayo, sisi Dimba kama wadau wa michezo wakongwe tunaozielewa harakati kama hizi za uchaguzi na hatima yake baada ya kumaliza zoezi, tunasisitiza tu kuwataka wanachama wawe makini kutumia kura zao. Tunafahamu kwamba zoezi hili halitarudia tena, hivyo makosa yoyote yatakayofanyika kitakachofuatia ni majuto tu yasiyokuwa na msaada. Tunajua kwamba, wanachama walioomba nafasi hizo walipata muda mzuri wa kufanya kampeni na kunadi sera zao, lakini katika uchaguzi wa klabu hizi kongwe mara nyingi lolote linaweza kujitokeza. Ndiyo maana tumeona umuhimu wa kuwakumbusha haya Wanasimba kwani tofauti na chaguzi nyingine zilizopita, huu unaielekeza klabu hiyo kongwe katika uendeshaji mpya chini ya kampuni ambao kamwe haitawezekana kufikiria kufanya mabadiliko kirahisi. Pamoja na yote sisi tunawaombe Wanasimba washiriki kwa amani uchaguzi huo na pia wapate viongozi watakaokuwa na msaada wa kuiendeleza klabu hiyo katika mtazamo wa kimataifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.