ULIZA UJIBIWE, UKURASA

Dimba - - NEWS -

Swali: Naitwa Godrey Elias wa Arusha, swali langu, yuko wapi kwa sasa kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger na anafanya nini? 0762426209

Jibu: Wenger raia wa Ufaransa aliyeinoa Arsenal kwa muda wa miaka 22, kabla ya kujiweka pembeni mwaka huu, yupo London, England, ingawa hajihusishi na masuala ya soka kama alivyobainisha wakati anaachana na washika mitutu hao. Swali: Naitwa Alphonce Lauleni wa Mtwara, nauliza ni mchezaji gani wa soka la Bongo analipwa fedha nyingi zaidi. 0685908264.

Jibu: Moja kati ya ugumu wa soka la hapa nyumbani kila kitu kinafanywa kwa siri mno, ni kama ilivyo upande huo wa mshahara wa wachezaji wetu ambao wanaupokea kwa mwezi tofauti na nchi nyingine ambazo kila kitu kinawekwa wazi.

Kinachofanywa na wahusika ambao ni viongozi wa klabu wanarahisisha tu majibu kusema mchezaji wa chini analipwa kiasi kisichopungua Sh 500,000, huku wanapokea mkwanja mrefu hasa wale wa kigeni si chini ya Sh milioni tano, hiyo ni kwa Simba, Yanga na Azam. Swali: Naitwa Issa Wazir wa Arusha, swali ni mkoa gani hapa Tanzania ambao una vipaji vingi vya mpira wa miguu? 0755366822.

Jibu: Kwa utafiti ambao si rasmi sana wa miaka ya karibuni, Morogoro ni miongoni mwa mkoa unaoonekana kutoa wachezaji wengi wenye vipaji wakiwamo Shiza Kichuya, Aishi Manula, Shomari Kapombe wote wa Simba.

Awali kabla ya nyota hao wa sasa, wakali wengine waliotokea viunga hivyo vya Mji kasoro bahari ni Ulimboka Mwakingwe, Juma Shaban, Jela Mtegwa, Gibson Sembuli, Zamoyoni Mogela na Malota Soma ‘Ball Jugller’.

Lakini pia Kigoma haiko mbali kwani huko ndiko walipotoka Juma Kaseja, Makumbi Juma, Abel Mziba, Edibul Lunyamila, Said Sued 'Scud' kama ilivyokuwa Mwanza kina Kelvin Yondan, Henry Joseph na Mrisho Ngassa. Swali: Naitwa Iman Mbani wa Kibaigwa, Dodoma, naomba kuuliza yuko wapi Mwafrika aliyetesa Ulaya miaka hiyo, George Weah na anashughulika na nini huko aliko. 0716622700

Jibu: George Tawlon Manneh Oppong Ousman Weah ambaye ni nyota pekee kutoka Afrika aliyefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia, Ballon d'Or, kwa sasa ni Rais wa taifa lao, Jamhuri ya Liberia tangu Januari 22, 2018. Swali: Naitwa Abdul Hassan wa Mbagala, Dar es Salaam, naomba kuuliza yuko wapi mchezaji wa zamani wa Simba, Ramadhani Chombo ‘Redondo’.0682467142

Jibu: Redondo timu yake kubwa ya Ligi Kuu Bara kuichezea mara ya mwisho ni Azam. Msimu uliopita alikuwa anaichezea Friends Rangers ya daraja la kwanza (FDL) ya Kinondoni chini ya Herry Mzozo. Swali: Eti mfungaji wa muda wote duniani ni Chitalu wa Zambia na si Lionel Messi wa Argentina.0674700969.

Jibu: Kwa mujibu wa wakusanya data kutoka RSSSF, orodha ya wafungaji 10 wa muda Aprili mwaka huu kinara ni Josef Bican raia wa Australia aliyefunga mabao 805 katika michezo 530 kwa muda wote aliocheza soka kuanzia 1931 hadi 1955.

Nafasi ya pili katika hiyo orodha inashikiliwa na Mbrazil, Romario aliyeingia kimiani mara 772, huku Cristiano Ronaldo akishika nafasi ya sita mabao 670 akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu, Messi mabao 635.

Hata hivyo, wakali wawili ambao wameendelea na kasi ya kuwaokotesha makipa mpira wavuni, Ronaldo na Messi bado wana nafasi kubwa ya kuongeza idadi ya mabao, lakini pia ikiwa imepita miezi saba tangu kutolewa kwa hiyo orodha. Swali: Naitwa Samwel Sai wa Kahama, Shinyanga, naomba kujua alipo mchezaji wa zamani wa Yanga, Juma Kampala, mimi ni msomaji wako mnazi wa gazeti la DIMBA. 0784120017

Jibu: Kampala alikuwa akicheza winga wa kushoto miaka ya nyuma katika kikosi cha mabingwa wa kihistoria, Yanga, hivi sasa ni mfanyakazi wa Hospital ya Taifa, Muhimbili (MNH). Swali: Naitwa Nasoro Songoro niko Kihinda, Morogoro, naomba kujua walipo miongoni mwa wachezaji hawa ambao walichezea klabu ya Yanga, Selestine 'Sikinde' Mbunga, Edger Fongo na winga Hussein Iddi.

Jibu: Mchezaji winga wa kushoto Selestine 'Sikinde' Mbunga ambaye pia alitamba akiwa na klabu ya Yanga, alikwishafariki dunia.

Mshambuliaji wa kati aliyevuma akiwa na klabu ya Yanga, Edger Fongo, hivi sasa anaishi Mwenge, jijini Dar es Salaam akishughulika na mambo yake binafsi.

Winga wa kulia, Hussein Iddi ambaye alitamba akiwa na klabu ya Yanga, hivi sasa yeye ni mkulima na anaishi Boko/Bunju, jijini Dar es Salaam. Swali: Naitwa Kondo Bwaza, TBT Matumbi, naulizia yuko wapi mchezaji wa zamani wa Simba, Ayoub Mzee.

Jibu: Mshambuliaji wa zamani wa kati aliyevuma akiwa na klabu ya Simba ,Ayoub Mzee, hivi sasa anaishi Tabata jijini Dar es Salaam ambako amejenga nyumba yake. Swali: Naitwa Ally Lyimo wa Karatu, Arusha, naomba nitajie vikosi vya Yanga na Simba vilivyocheza Nyamagana, Mwanza mwaka 1974 na wafungaji wa mechi hiyo kwa pande zote mbili.

Jibu: Mechi hiyo ambayo ilikuwa ni kali na ya kusisimua kwa muda wa dakika 120, Yanga waliibuka washindi kwa kuifunga Simba mabao 2-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na Gibson Sembuli (marehemu) katika dakika ya 87 na Sunday Manara ‘Computer’ katika dakika ya 97, huku bao pekee la Simba likifungwa na Adam Sabu (marehemu) katika dakika ya 16.

Kikosi cha Yanga kiliwakilishwa na Michael Elias (marehemu)/ Muhidin Fadhili, Seleiman Sanga (marehemu), Boi Wickens (marehemu), Hassan Gobbos, Omari Kapera (marehemu), Abdulrahman Juma (marehemu), Leonard Chitete (marehemu), Sunday Manara ‘Computer’, Kitwana Manara ‘Popat’, Gibson Sembuli (marehemu) na Maulid Dilunga (marehemu).

Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na Athumani Mambosasa (marehemu), Shabaan Baraza, Mohamed Kajole ‘Machela’ (marehemu), Jumanne Masmenti (marehemu), Omari Chogo (marehemu), Omari Gumbo, Willy Mwaijibe (marehemu)/Adam Sekulu, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu (marehemu), Abdallah ‘King’ Kibadeni na Saad Ally.

NA MAREGES NYAMAKA

0653- 042 018

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.