Mwenye namba yangu nimerudi

Dimba - - NEWS - NA JESSCA NANGAWE

MOJA ya mabeki imara ndani ya kikosi cha Yanga ni pamoja na Juma Abdul. Beki huyo wa kulia amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kwa zaidi ya misimu mitatu iliyopita kupitia Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa. Tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu, Juma Abdul, amekuwa mwenye kujiuguza majeraha ya goti ambayo yamemlazimu kupokwa namba na kinda Paul Godfrey aliyeaminiwa na kocha Mwinyi Zahera. Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba sasa Juma Abdul amerejea kazini na leo yumo kwenye kikosi cha kwanza kitakachoanza mchezo dhidi Ndanda FC Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kurudi kwa Juma kunaibua vita ya namba dhidi ya Paul Godfrey ambaye ameonyesha kumudu nafasi hiyo lakini kwa bahati mbaya leo hatakuwemo kwenye kikosi kwa sababu ya kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata mchezo uliopita wa Ligi Kuu. DIMBA limefanya mahojiano na beki huyo kuhusu kurejea kwake upya mzigoni na kuelezea undani wa majeraha yaliyokuwa yakimkabili na vita ya namba ndani ya kikosi cha timu hiyo.

DIMBA: Pole na majeraha yaliyokuwa yakikukabili?

JUMA ABDUL: Ahsante nashukuru Mungu nimepona na kama kocha itampendeza leo nitakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoanza kwani mwenye namba yake amerudi. DIMBA: Tatizo lilikuwa nini hasa? Lilisababishwa na nini?

JUMA ABDUL: Nilikuwa nasumbuliwa na goti kwani kuna nyama ilikuwa imepasuka ambayo ilinilazimu kukaa nje kwa muda huku nikijitibu na nashukuru Mungu hali yangu inaendelea vizuri.

DIMBA: Unaamini tatizo lako limekwisha? JUMA ABDUL: Naamini limekwisha..lakini kikubwa unajua hapa kwetu hatuna utaratibu mzuri wa kutibiwa majeraha yetu na ndio maana wachezaji wengi wanapoumia na kulazimika kukaa nje basi ni wachache wanaoweza kurudi kwenye viwango vyao. DIMBA: Mashabiki wanakumfuatilia tamani kujua umerudi na mikakati ipi katika kuhakikisha kikosi changu kinarejesha heshima ya ubingwa msimu huu?

JUMA ABDUL: Kwanza namshukuru Mungu kwa kurejea vyema hali yangu, kwa sasa ni mapema kuzungumzia ubingwa kwa kuwa ndio kwanza tunaingia mchezo wa raundi ya tisa. Yote kwa yote mikakati yetu ni kuhakikisha tunarejesha heshima Jangwani kwa kuwapoka Simba ubingwa msimu huu.

DIMBA: Unazungumziaje ushindani wa namba hasa nafasi yako ambayo Paul Godfrey alikuwa akiishikilia?

JUMA ABDUL: Ushindani wa namba ni muhimu na ndio maana unaona kila mchezaji anajituma ili kumshawishi mwalimu, ukiangalia huyu dogo amejituma na ndio maana kocha amemkubali na kumpa nafasi, naamini tutaendeleza hilo kwa masilahi ya timu na sisi wenyewe.

DIMBA: Unamzungumziaje kocha Zahera? JUMA ABDUL: Zahera ni kocha mzuri, ameanza vizuri na timu na nategemea ataifikisha mbali kutokana na falsafa yake ndani ya nje ya uwanja, nadhani wachezaji wenzangu tungempa nafasi na kumpa ushirikiano wa kutosha zaidi. DIMBA: Ulijisikiaje baada ya kuukosa mchezo wenu dhidi ya Simba msimu huu?

JUMA ABDUL: Kama mchezaji nilijisikia vibaya, unajua mechi za derby ndio za kuonyesha kiwango chako kiko wapi, pale ndio sehemu ya mawakala kukuona, ukweli nilisikitika lakini nilijipa moyo na nashukuru wachezaji wenzangu hawakuniangusha ingawa matokeo yalikuwa vile.

DIMBA: Unamzungumziaje kinda wenu mpya, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto? JUMA ABDUL: Ni mchezaji mwenye uwezo, ana bidii na nimtiifu, nilianza si tu baada ya kuja Yanga, tangu akiwa kwao Zanzibar, niliona uwezo wake, namshauri asibweteke na hizi timu, apambane kutimiza ndoto za kufika mbali na atafanikiwa katika hilo.

DIMBA: Unakionaje kikosi cha wapinzani wenu msimu huu?

JUMA ABDUL: Simba ni wazuri na wana kikosi kipana, si Simba tu sasa hivi tuna timu 20 kwenye ligi, zote zina ushindani naamini msimu huu ushindani ni mkubwa na hata bingwa atapatikana katika mazingira magumu. DIMBA: Wewe ni shabiki wa timu gani Ulaya na ni mchezaji gani ni role model wako? JUMA ABDUL:

Mimi naipenda sana timu ya Manchester United na namkubali sana Daniel Alves na Cristiano Ronaldo, wamekuwa wakinishawishi na kunipa moyo wa kucheza mpira hadi sasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.