TAMTHILIA ILIYOBAMBA NCHI 40 DUNIANI

Dimba - - NEWS - NA BRIGITTE EMMANUEL

LICHA ya kwamba tumekuwa tukiwaletea simulizi ya tamthilia ya Sultan katika gazeti hili, lakini wasomaji wetu wengi ambao wamekuwa wakiifuatilia kupitia kituo cha televisheni cha Azam kupitia chaneli yake ya Azam Two wameomba tuwaletee kwa ufupi sana simulizi ya tamthilia hiyo kuanzia mwanzo hadi ilipo sasa ili waweze kwenda nayo sambamba. Hii ni kutokana na baadhi yao kuikutia njiani hivyo kushindwa kujua mtiririko wa hadithi nzima hadi ilipo sasa. Na kwa kuwa tunawapenda wasomaji wetu na hasa ukizingatia kuwa ndiyo tamthilia inayobamba kinoma mjini kwa hivi sasa kiasi cha kuwafanya watu wengi kuifuatilia tumeona tutekeleze ombi lao. DIMBA linafahamu kuwa wengi watakaoisoma kuanzia sasa na baadaye kuendelea na mtiririko mzima wata enjoy vya kutosha. Pata uhondo kamili...

UTANGULIZI...

SULTAN ni tamthilia ya Kituruki iliyorushwa ama inayoendelea kurushwa katika nchi zaidi ya 40 duniani. Ikiwa imeandikwa na mtunzi mahiri anayeheshimika ulimwenguni, Meral Okay, akisaidiana na Yilmaz Sahin, ni tamthilia inayozungumzia maisha ya mfalme wa dola ya Ottoman, Suleyman, anayesifika kuwa bora zaidi kati ya Wafalme wa enzi hizo pamoja na mkewe Hurrem Sultan, binti mtumwa aliyegeuka kuwa malkia.

Akiwa na umri wa miaka 26, wakati utawala wake ulipoanza, Sultan Suleyman alifikiria kujenga dola imara na kubwa zaidi kuliko hata ile ya Alexander The Great (Alexander Mkuu).

Huyu alikuwa ndiye mfalme wa Masedonia, ambako ni Kaskazini mwa Ugiriki (kuanzia mwaka 336 – 323 KK) na anajulikana kama mmoja kati ya amiri jeshi waliofanikiwa kupita wote wengine katika historia ya dunia. Kabla hajafariki akiwa na umri wa miaka 33 aliteka sehemu kubwa ya dunia iliyojulikana na Wagiriki wa zamani zake, kuanzia Ulaya hadi Bara Hindi na Misri.

Lakini Sultan Suleyman, ambaye alitawala Uturuki katika kipindi cha miaka 46, ni kama vile alimfunika kutokana na umaarufu wake kama shujaa mkuu na mwenye mafanikio ambaye sifa zake zilienea kila sehemu duniani.

Huku akishirikiana na rafiki yake wa tangu utotoni, Pargali Ibrahim, ama Ibrahim Pasha, Suleyman alipata ushindi katika vita nyingi za kijamii na kiuchumi hivyo kujikuta akizidi kujizolea umaarufu hasa katika dunia ya Uislamu.

Suleyman alimchukulia Ibrahim Pasha kama ndugu yake wa damu, rafiki na mshauri mkuu. Kutokana na heshima hiyo, aliweza kumpa dada yake Hatice Sultan, kuwa mkewe hivyo kwa upande mwingine wawili hawa walikuwa ni mashemeji.

Simulizi ya tamthilia ya Sultan inamwonyesha Suleyman alivyokuwa na nguvu katika utawala wake, akimtumia Ibrahim Pasha kama Waziri wake mkuu ambaye alianzisha utawala wa sheria katika dola hiyo tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kutokana na cheo cha Uwaziri Mkuu, Ibrahim Pasha, ndiye pia aliyekuwa na jukumu la kushughulikia masuala ya kidiplomasia kwa maana ya kukutana na viongozi wa dola mbalimbali za nje huku pia akiwa ndiye mwandaaji mkuu wa kampeni za kijeshi ikiwemo kuongoza vita, hasa katika kipindi hicho ambacho kulikuwa na upinzani kati ya Uislamu na Ukristo pamoja na kutetea dola yao ya Ottoman.

Tamthilia hiyo pia inaangazia mahusiano miongoni mwa wananchi wa dola ya Ottoman, wanafamilia wa kifalme na wengineo hususan katika masuala ya kijamii, kimapenzi na migogoro.

Pia kuna mgogoro kati ya Hurrem Sultan na Mahidevran Sultan, mama wa mtoto mkubwa wa kiume wa Sultan Suleyman na majukumu ya Hafsa Sultan, mama wa Suleyman; kuibuka kwa Hurrem hadi kuwa chaguo la kwanza hasa baada ya kupata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza wa kiume, kuporomoka kwake na kurejea tena kwenye neema, mahusiano ya Pasha Ibrahim na Hatice Sultan, dada wa Suleyman na mengine mengi tu.

PICHA NZIMA IKO HIVI....

Tamthilia hii inaanzia mwaka 1520, ambapo mwana wa mfalme wa Manisa, 'Prince Suleyman' anapata taarifa za kifo cha baba yake wakati akiwa kambini na anatakiwa kuripoti haraka katika mji mkuu wa Uturuki Istanbul, ambako angekabidhiwa cheo cha kuwa Mfalme wa 10 wa dola ya Ottoman.

Akiwa na rafiki yake kipenzi wa tangu utotoni, Pargali Ibrahim a.k.a. Ibrahim Pasha, Suleyman anasafiri hadi Constantinople kwenda kurithi Ufalme wa baba yake.

Wakati huo huo, meli ya mizigo iliyokuwa imebeba watumwa kutoka ng'ambo ya pili ya Bahari nyeusi (The black sea) katika nchi ya Crimea, ambayo kwa sasa ndiyo Ukraine, inatua nanga nchini Uturuki na miongoni mwa watumwa hao yumo mmoja aitwaye Alexandra La Rosa (Hurrem), ambaye alitekwa enzi za utumwa wa Tatar, huko Ruthenia.

Tabia yake ya upinzani na ukorofi na kutoheshimu wamiliki wake, inamfanya aondolewe miongoni mwa watumwa na kujikuta akiletwa nchini Uturuki.

Kwa upande mwingine, Suleyman anawasili Constantinople na kumsalimia mama yake, Ayse Hafsa, pamoja na dada yake mdogo Hatice Sultan.

Bila kupoteza wakati, anaapishwa na kukabidhiwa kuwa Sultani, ama mfalme wa dola ya Ottoman.

Alexandra (Hurrem) na watumwa wengine wanauzwa Topkapi, kwenye jumba la kifalme na wanakaguliwa na daktari wa kike.

Kutokana na urembo wake pamoja na ushupavu aliokuwa nao, Alexandra anajikuta akiwa miongoni mwa wanawake wanaoteuliwa kumhudumia Sultan Suleyman.

Tabia yake ya ukorofi inawasikitisha watumwa wenzake na kuzifanya habari zake kumfikia mama wa Sultan, Hafsa Sultan.

Mama wa Sultan (Hafsa Sultan) anamvaa Alexandra na kumweleza kuwa sasa yeye ni mali ya Sultan na kwamba kuendelea kuwa na tabia mbaya kutasababisha aadhibiwe.

Alexandra anagoma kusikiliza na kudai kwamba yeye si mali ya mtu yeyote na hivyo kuendelea na tabia zake za kipinzani.

Nigar, mtumwa na msimamizi mkuu wa watumwa wa kike ndani ya jumba la mfalme ambaye pia ni mpenzi wa Ibrahim, anaonekana kuvutiwa na Alexandra na kumwambia kuwa kama anataka kufanikiwa ndani ya jumba lile, basi anapaswa kuheshimu sheria za mle ndani na hata kama akitakiwa kulala na mfalme na kwa bahati nzuri akashika mimba, ataitawala dunia kama Haseki Sultan.

Alexandra anaanza kutamani kufanya kila njia ili Sultan Suleyman aweze kuujua urembo na uwepo wake.

Anafanikiwa kuanza kumteka taratibu. Na hii ni baada ya kupata habari zake kupitia kwa watumwa wengine. Hata hivyo, baadaye anaizuia nafsi yake na kujaribu kumsahau.

Ni nini kinaendelea? Nunua gazeti la DIMBA toleo la Jumatano ili uweze kufuatilia vizuri simulizi ya tamthilia hii ya kusisimua.

WAHUSIKA WA LEO

Hurrem Sultan Jina kamili: Meryem Sahra Uzerli

Hurrem Sultan ndiye mhusika mkuu wa tamthilia hii. Jina lake kamili ni Meryem Sahra Uzerli. Meryem Uzerli alizaliwa Agosti 12, huko KasselWilhelmshohe, nchini Ujerumani. Baba yake aitwaye Huseyin, ni Mturuki wakati mama yake ambaye jina lake ni Ursula, yeye ni raia wa Ujerumani. Anao ndu- gu zake wakubwa watatu wakiwemo kaka zake wawili pamoja na dada yake aitwaye Canan, ambaye ni mwanamuziki wa muziki wa jazz.

SULTAN SULEYMAN

Jina kamili: Hatic Ergenc Jina kamili la Sultan Suleyman ni Hatic Ergenc. Halit Ergenc alizaliwa kwenye familia ya mwigizaji Sait Ergenc Aprili, 1970, huko Istanbul, Uturuki.

Alimaliza elimu yake ya sekondari huko Besiktas Atatürk High School, mwaka 1989 na kuingia Chuo Kikuu cha Ufundi cha Istanbul, kwa ajili ya kusomea masomo ya uhandisi wa meli. Aliachana na masomo hayo mwaka mmoja baadaye na kuamua kusomea masuala ya kompyuta akihusika zaidi na idara ya masoko pia. Pia alikuwa ni mwimbaji mwitikiaji na mcheza shoo wa Ajda Pekkan na Leman Sam.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.