Majeruhi mwingine Arusha afanyiwa upasuaji

Mtanzania - - Mbele - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MTOTO Doreen Mshana amefanyiwa upasuaji mkubwa wa uti wa mgongo kwa saa tano nchini Marekani anakotibiwa.

Wakati anaingizwa kwenye chumba cha upasuaji alasiri jana, madaktari wanaomtibu waliwataka Watanzania wamuombee Mungu amponye.

Doreen ni miongoni mwa watoto watatu walionusurika katika ajali ya basi la Shule ya Msingi ya Lucky Vicent ya Arusha.

Watoto hao, Doreen, Saidia Ismail na Wilson Tarimo walikuwa katika basi hilo ambalo lilitumbukia korongoni Mei 6 mwaka huu katika eneo la Karatu mkoani Arusha na kuua wenzao 32, walimu wawili na dereva.

Madaktari wa kujitolea wa taasisi ya elimu ya afya ya STEMM (Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries), walikuwa miongoni mwa watu waliofika mapema eneo la tukio na kushiriki shughuli za uokoaji.

Madaktari hao ndiyo waliowasafirisha majeruhi hao watatu Mei 14 mwaka huu kwenda Marekani kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Mercy.

Juzi, tovuti ya siouxcity.com iliripoti kuwa ajali hiyo ilivunja mifupa minne ya pingili za uti wa mgongo wa Doreen na kwamba alipooza kuanzia kiunoni kwenda chini.

Dk. Steve Meyer ambaye pia ni Rais wa STEMM, alikaririwa na tovuti hiyo akisema kuwa Doreen anaweza kutingisha kidogo kidole cha mguu wa kushoto.

Katika ukurasa wake wa Facebook jana, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa STEMM, alisema Doreen alikuwa ameingizwa chumba cha upasuaji katika Hospitali hiyo ya Mercy tayari kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

“Mungu amtendee uponyaji mtoto Doreen,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.