Ugonjwa wa mtoto anayekunywa mafuta kutajwa leo MNH

Mtanzania - - Mbele - Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

JOPO la madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) waliomfanyia vipimo vya uchunguzi mtoto, Shukuru Kisonga (pichani), leo litatoa ripoti kueleza kile walichokibaini.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 16 amekuwa akilazimika kula mafuta ya kula lita moja, maziwa lita mbili na robo tatu ya kilo ya sukari ili aishi kama watu wengine na akivikosa vitu hivyo hupata maumivu makali mwilini.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, alisema uchunguzi wa madaktari umekamilika.

“Juzi walimchukua damu na kufanya vipimo mbalimbali, ilikuwa watoe taarifa hiyo leo (jana) lakini wameomba waitoe kesho (leo),” alisema.

Shukuru na mama yake, Mwanabibi Mtete, walifika Hospitalini kutoka nyumbani kwao Tunduru mkoani Ruvuma kwa agizo la serikali baada ya taarifa zake kusambaa katika mitandao mbalimbali ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwanabibi alisema iwapo Shukuru akikosa vitu hivyo vitatu mwili wake huwa kama gari lililoishiwa mafuta.

“Huwa anapata maumivu makali, anakuwa kama anajikata kata, natumia mikono yangu kumsaidia, sasa mimi ni mjane maisha yangu ni duni nilikuwa napata wakati mgumu kumsaidia mwanangu,” alisema.

Alisema Shukuru ni mwanafunzi wa kidato cha pili wilayani humo na hali hiyo inapomtokea wenzake shuleni hulazimika kumbeba na kumrudisha nyumbani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.