Raia wapya wazaliana ovyo

Mtanzania - - Mbele - Na TIGANYA VINCENT -KALIUA

WATANZANIA wapya ambao walikuwa wakimbizi wa Burundi wanazaliana bila mpango kutokana na kukosa elimu juu ya suala hilo, imebainika.

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Balozi Celestine Mushi aliomba mashirika ya kimataifa na Umoja wa Ulaya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwasaidia Watanzania kuona umuhimu wa kuwaunganishwa na jamii ya Watanzania baada ya kupata uraia.

Balozi Mushi alitoa wito huo jana katika eneo la Ulyankulu wilayani Kaliua alipokuwa na ujumbe wa mabalozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ikiwamo Uingereza.

Alisema kukosekana elimu ya kutosha kumewafanya watanzania hao wapya wawe na familia kubwa ambazo hawawezi wakati mwingine kuziwezesha katika huduma za jamii.

Balozi Mushi alisisitiza kuwa kutozingatiwa kwa elimu ya uzazi wa mpango kumelifanya eneo hilo kuwa na wananchi wanaozaliana kwa wingi kuliko maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.

Alisema jambo hilo linafanya huduma za jamii kuwa kidogo ikilinganishwa na idadi ya watu waliopo.

“Kimsingi raia hao wapya wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo ukosefu wa maji safi na salama, uhaba wa vifaa tiba, zahanati, kutokuwa na miundombinu ya kutosha ya elimu na kukosa elimu ya kutosha kuhusu uzazi wa mpango.

Alisema baada ya Serikali kuwapatia waliokuwa baadhi ya wakimbizi wa Burundi uraia ni vema nchi hizo na mashirika ya kimataifa yakasaidia kuongeza raslimali ambazo zitaisaidia Serikali iweze kuwaunganisha vizuri raia hao wapya na raia wengine nchini. Balozi Mushi aliongeza, “Fedha za Serikali pekee hazitoshi kukamilisha hatua ya kuwaunganisha raia hao kwa sababu yapo mahitaji ya wananchi yanayotegemea hizo fedha kidogo inazokusanya kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato na hivyo ni vema nao wakasaidia kwa upande wao”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kaliua, Dk. John Pima alisema raia katika eneo la Ulyankulu wanazaana kwa asilimia 5.4 na hivyo kufanya kuwapo watu wengi katika eneo moja ambao hawawiani na huduma za jamii zilizopo. Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Huduma ya Wakimbizi, Suleman Mziray, alisema ujumbe huo wa mabalozi ulikuwa Ulyankulu kujionea hali halisi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.