Mwijage awatoa hofu wabunge

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU -DODOMA

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema wizara yake ina mawasiliano mazuri na Wizara ya Fedha na Mipango.

Kutokana na hali hiyo, amesema wabunge hawana haja ya kuwa na hofu juu ya hilo, ingawa baadhi yao wanaonekana kuhofia uhusiano huo.

Waziri Mwijage aliyasema hayo juzi, wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18 aliyoiwasilisha juzi.

“Kuna jambo hapa limezungumzwa na wabunge wengi, kwamba wizara yangu haina mawasiliano mazuri na Wizara ya Fedha. Ukweli ni kwamba, jambo hilo halipo kwa sababu mawasiliano serikalini ni mazuri sana.

“Kwa kawaida, serikali inawasiliana kwa barua na ndiyo maana kuna barua ninazo ambazo nimekuwa nikiwasiliana na Waziri wa Fedha, ila siwezi kuzitoa hapa kwa sababu ni za siri.

“Kwa hiyo, waheshimiwa wabunge mliokuwa mnasema wizara yangu haina mawasiliano na wizara hiyo, eleweni kwamba serikalini kuna mawasiliano mazuri,” alisema Mwijage.

Akizungumzia viwanda, Waziri alisema sekta hiyo imegawanyika katika maeneo mbalimbali kutokana na ukubwa wa kiwanda.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wabunge waendelee kuiamini Serikali kwa kuwa ina nia njema ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini ambayo alisema sehemu kubwa ya wabunge waliyalalamikia, alisema ni mazuri kwa kuwa Tanzania ni ya 144 kati ya nchi 190 duniani.

Alikiri kuwa, pamoja na sekta ya viwanda kwa sasa kuanza kufanya vizuri, bado kuna haja ya kuhakikisha uwekezaji unaongezeka na kuanzisha viwanda mbalimbali muhimu, vikiwamo vya madawa.

“Tuna aibu nyingi kwa kweli, lakini nawahakikishia zote tutazifuta, kwa sasa tunaagiza hadi dripu, hii ni aibu, nawaahidi tutajenga viwanda.

Mimi si saizi ya kuzalisha viwanda vyenye thamani ya Sh trilioni tano tu kwa mwaka mmoja,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.