Wanafunzi vyuo 11 kupigwa ‘msasa’ leo

Mtanzania - - Mkoa - Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Trust Care Tanzania Foundation limeandaa semina maalumu ya siku moja kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu 11 vilivyopo jijini kwa lengo la kuwajenga kifikra ili kuweza kuzitumia fursa zinazowazunguka kutimiza ndoto zao.

Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, ambalo si la kiserikali, Zambert Mbwafu, alisema semina hiyo itakayofanyika leo katika ukumbi wa Chuo cha Elimu Kishiriki (DUCE), imeandaliwa kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya TTCL, ambapo pamoja na mambo mengine, ina lengo la kuwajenga vijana kifikra kuwa na mawazo chanya na kuzitumia fursa mbalimbali.

“Katika semina hiyo mambo yatakayojadiliwa zaidi ni umuhimu wa kujiamini na kujijengea uwezo, uwezo wa uthubutu, vipaji na jinsi ya kuviendeleza, maadili na nidhamu katika kazi na ubunifu katika kufikia malengo,” alisema Mbwafu.

Alisema semina itawaandaa vijana waliopo na wanaotarajia kumaliza elimu ya juu hivi karibuni kupata elimu ambayo itawasaidia wakiwa shule na baada ya kumaliza masomo.

Alisema lengo ni kuwasaidia kuweza kwenda sambamba na mahitaji ya dunia katika kuleta maendeleo na kupambana na changamoto za kimaisha ndani na nje ya mipaka.

Alisisitiza shirika hilo limewaalika wasomi pamoja na watu mbalimbali waliothubutu kufanya masuala mbalimbali, akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Joel Kayombo, mwanzilishi wa Mkuyuni Foundation Sylvester Jotta na wengineo.

Vyuo vitakavyoshiriki semini hiyo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBE), Chuo cha Uhasibu (TIA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Tiba Muhimbili (MUHAS), Chuo cha Diplomasia na vinginevyo.

Mambo yatakayojadiliwa zaidi ni umuhimu wa kujiamini na kujijengea uwezo wa uthubutu. – Zambert Mbwafu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.