Wachimbaji wawili wafariki mgodini Iringa

Mtanzania - - Mkoa - Na FRANCIS GODWIN

WACHIMBAJI wawili wadogo wa madini katika Kijiji cha Masuluti, Kata ya Magulilwa, Tarafa ya Mlowa, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, wamefariki dunia baada ya kukosa hewa ndani ya mgodi.

Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Masuluti, Venjaslaus Kiunosile, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi.

Alisema kuwa, taarifa ya tukio hilo alipewa na mchimbaji mwenzao aliyewatembelea marehemu hao kwa ajili ya kuwasalimia.

Mtendaji huyo alisema kutokana na taarifa hiyo walilazimika kutoa taarifa polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa miili ya marehemu hao imetolewa katika mgodi huo.

Aliwataja waliofariki dunia kwa kukosa hewa kuwa ni Haus Kaijage (32), mkazi wa Bukoba na James Mlawa (22), mkazi wa Magulilwa.

Alisema chanzo cha watu hao kupoteza maisha ni kukosa hewa, baada ya kuingiza jenereta la kuvuta maji mgodini kwa lengo la kuvuta maji na baada ya kuliwasha walikosa hewa.

Alisema wachimbaji hao walichukua mashine hiyo na kuingiza ndani ya mgodi baada ya awali kuharibika na kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano mmiliki wa mgodi huo, Samweli Msigwa.

Kamanda Mjengi alitoa wito kwa wachimbaji wadogo katika Mkoa wa Iringa kuzingatia usalama katika uchimbaji wa madini.

Amina Masenza

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.