Ripoti waliotafuna mali za Nyanza yatua kwa Magufuli

Mtanzania - - Kanda - Na BENJAMIN MASESE

RAIS Dk. John Magufuli amekabidhiwa ripoti maalumu ya uchunguzi wa mali za Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU) 1984 Ltd, zilizouzwa na kununuliwa kinyemela na vigogo.

Taarifa ya kukabidhiwa ripoti hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Leonard Masale, alipofungua Mkutano Mkuu wa 25 wa NCU na kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 500 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Dk. Masale alisema kazi ya uchunguzi wa jinsi mali za NCU zilivyonunuliwa, kuuzwa ama kuporwa na watu wenye ukwasi umekamilika kama ilivyoagizwa Agosti 11, mwaka jana na kinachosubiriwa ni maelekezo kutoka kwake.

Alisema kazi ya uchunguzi wa mali hiyo ilikuwa ngumu, lakini Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na timu yake chini ya vyombo vya usalama ilifanikisha kuifanya kwa umakini na uadilifu mkubwa hadi ilipokamilisha na kuikabidhi hivi karibuni kwa Magufuli.

“Hadi sasa kinachosubiriwa ni maelekezo kutoka kwa Magufuli, maana timu ya uchunguzi imekamilisha kazi iliyopewa na Rais, tusifichane, kazi hii ilikuwa ngumu kidogo maana waliokwapua mali hizo walikuwa na ukwasi mkubwa na ushawishi wa aina yake.

“Kama mnakumbuka baada ya sakata hili kuanza, hata uongozi uliokuwapo ulianza kugawanyika na hata kila mmoja kufanya kazi anavyojua, ndiyo maana uliondolewa haraka madarakani na kuteuliwa wengine ambao mnawaona hapa, hivyo mali zenu ziliuzwa na wachache kwa maslahi yao.

“Niwahakikishie kwamba tuwe na imani na Magufuli kwamba maelekezo yake yatakuwa ya tija na pengine mali zote zitarejea, kwa kila mmoja wetu anapaswa kuushukuru utawala wa awamu ya tano, maana umejikita kuwasaidia wanyonge na kuvisaidia vyama vya ushirika kama ilani ya CCM inavyosema,” alisema.

Pia alisema taarifa iliyofikishwa kwa Magufuli inahusu mali za NCU ya New Era, Vick Fish, majengo ya Kauma, viwanja vya Isamilo na maghala ya Igogo.

Aliwataka wanachama wa NCU kuhakikisha wanapandisha uzalishaji wa pamba ili usiendelee kushuka kila mwaka, huku akitolea mfano kuwa katika msimu wa mwaka 2015/2016, tani 250,000 ndizo zilipatikana, huku msimu wa mwaka 2016/2017 zilivunwa tani 150,000, pungufu ikiwa tani 100,000.

Alisema chanzo cha kushuka kwa zao hilo ni wakulima kutopewa mbegu bora, pia bei ndogo iliyotokana na uwepo wa madalali ambao hivi sasa wamepigwa marufuku na Serikali.

Awali, Kaimu Meneja wa NCU, Juma Mokiri, alisema chama hicho kimekusudia kufufua viwanda 10 vya kuchambua pamba na viwanda vitano vya mafuta yatokanayo na zao hilo.

Alisema viwanda hivyo vitafufuliwa kwa awamu kwa kushirikiana na wabia kutoka kampuni ya Bajaji, huku akifafanua kuwa wanaanza na viwanda viwili vitakavyogharimu Sh bilioni 2.4 chini ya usimamizi wa Serikali.

Naye Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Charles Malunde, aliwataka wanachama wa NCU kukataa kutawaliwa kimawazo na kujipanga kuhakikisha chama hicho kinakuwa imara kwa kununua mazao wenyewe na kumiliki viwanda.

Niwahakikishie kwamba tuwe na imani na Magufuli kwamba maelekezo yake yatakuwa ya tija na mali zitarejea – Dk. Leonard Masale

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.