Jela miaka 120 kwa ubakaji, unyang’anyi

Mtanzania - - Kanda - Na AHMED MAKONGO

MAHAKAMA ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara imewahukumu Nsimba Chacha (26), mkazi wa Mtaa wa Nyakato na Wambura Mussa (46) mkazi wa Mtaa wa Rwamlimi, kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 120 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 16 kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Karim Mushi, baada ya kuridhika bila kuacha shaka yoyote na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

“Kwa kila kosa mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela, ambapo kwa makosa yote mawili, yaani unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba ni jumla ya miaka 60 na hivyo kufanya jumla ya miaka 120 kwa washtakiwa wote wawili.

“Kwa vile adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na nimetoa adhabu hiyo baada ya kuupitia ushahidi huo na kisha kutafsiri sheria na kwamba adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa washtakiwa hao na watu wengine wanye nia au tabia ya kutenda makosa kama hayo,” alisema Hakimu Mushi.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Jonas Kaijage na Mwanasheria wa Serikali, Frank Nchanila, kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja walitenda makosa hayo Mei 29, mwaka 2009 saa 5:00 usiku katika eneo la Mtaa wa Nyakato, mjini Musoma.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio washtakiwa hao wakiwa na silaha mbalimbali walivamia nyumbani kwa Ramadhan Meledi, mkazi wa Nyakato mjini Musoma na kufanikiwa kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 995,000.

Aidha, ilielezwa kuwa, baada ya kufanya uporaji huo, pia watu hao walimbaka kwa zamu binti mmoja (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16 na kumwachia maumivu makali na kisha wao wakatokomea kusikojulikana.

Kaijage na Nchanila walisema washtakiwa hao wote kwa pamoja walitenda makosa hayo kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 na baada ya kufanya unyama huo walitokomea kusikojulikana, lakini baadaye walikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani hapo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.