Zahanati Ulowa yakabiliwa na ufinyu chumba cha CTC

Mtanzania - - Kanda - Na PASCHAL MALULU

UFINYU wa chumba cha kutolea ushauri nasaha (CTC) katika Zahanati ya Kata ya Ulowa, katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, umesababisha wagonjwa kushindwa kutoa siri za magonjwa yao ya kuambukiza kwa waganga wa kituo hicho.

Hayo yameelezwa jana na Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Bulungwa, Esther Matone, wakati akichangia katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo, kilichofanyika katika Kata ya Nyamilangano, ambako ndipo makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Matone alisema amekuwa akipiga kelele kuhusu suala la kuongezwa kwa ukubwa wa chumba hicho ili kuwafanya wagonjwa wawe na uwezo wa kusema matatizo yao bila mtu yeyote kuweza kusikiliza siri ya maradhi yanayomkabili bila kupata majibu ya kina.

Naye Diwani wa Kata ya Ulowa, Paschal Mayengo, alilieleza baraza hilo kuwa, Zahanati hiyo ilijengwa na wananchi wa kata hiyo, ambapo vyumba hivyo havikukidhi vipimo vya ujenzi na kudai kuwa chumba kimoja upana na urefu ni mbili kwa mbili, ukilinganishwa na chumba chenyewe cha mapokezi.

“Pamoja na ufinyu wa chumba cha kutolea ushauri nasaha (CTC), Kata ya Ulowa ina jumla ya wakazi wapatao 20,000 ambao wanatibiwa katika zahanati hiyo, ambayo pia hupokea wagonjwa kutoka kata za jirani za Ubagwe pamoja na Kaliua ya mkoani Tabora na hivyo halmashauri inapaswa kuona umuhimu wa kupanua chumba hicho pamoja na zahanati yenyewe,” alisema Mayengo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Matomoro Michael, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa madiwani hao, hivyo alitumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji katika halmashauri hiyo kulitafutia ufumbuzi, huku akisema kuwa, zahanati za Ulowa na Ulewe zinakabiliwa na changamoto hiyo ya vyumba vya kutolea ushauri nasaha (CTC).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.