Pam Grier alivyochukua pointi tatu, 1973- 83

Mtanzania - - Swaggaz -

N IMEGUNDUA kitu kimoja, kwamba kumbukumbu nyingi zinazosisimua mashabiki wetu ni zile zinazohusu muziki wa disko na pia filamu, hasa zile sinema za kibabe na wakati mwingine zinazohusu mapenzi mazito.

Ndiyo maana nikajiridhisha kwamba, ili twende sawa hapa lazima niwatafute waigizaji waliowahi kutengeneza sinema za aina hii.

Bahati nzuri ndani ya Kijaruba kumesheheni kila kitu, ukiwataka akina Christopher Lee wamo humo, Leon Isaac Kened, Susan Mellow, Michael Wolker na wengine ilimradi tukumbushane mambo yalivyokuwa mazuri enzi hizo.

Leo nimeamua kurudi nyuma sana na kumkuta mkali mmoja wa Sinema aliyewahi kutikisa ulimwengu anayekwenda kwa jina la Pam Grier.

Sitaki kumsahau mwigizaji huyo raia wa Marekani anayejulikana kwa majina mengine Pamela Suzette lakini aka “Pam” Grier aliyezaliwa Mei 26 mwaka 1949, hii inatokana na kazi alizowahi kufanya katika kipindi cha ujana wake.

Mkali huyo alitikisa hasa Jiji la Dar es Salaam, miaka 10 tangu alipoigiza katika picha moja kali iitwayo Black Mama and White Mama, kazi iliyowavutia kupita kiasi mashabiki wa filamu enzi hizo.

Lakini aliwahi pia kufanya kazi nyingine kubwa katika filamu za The Big Bird Cage (1972), Coffy (1973), Foxy Brown (1974) na Sheba Baby aliyoitendea haki mwaka (1975).

Lakini kazi niliyokusudia kuwakumbusha wasomaji ni ile niliyoitaja hapo juu, ambayo iliyafanya majumba ya sinema miaka hiyo Empire, Empress, New Chox, Avalon. Odeon, Cameo na Star Light, haikuwahi kuonyeshwa Drive Inn kutokana na jumba hilo lilikuwa wazi hivyo sinema zilizohusika kuangaliwa na watu wazima pekee hazikuruhusiwa.

Akishirikiana na mkurugenzi Eddie Romero na mtayarishaji maarufu enzi hizo John Ashley, Pam Grier aliiwezesha filamu yake kuonekana kama ni matukio ya ukweli na siyo kuigiza kama zilivyo filamu nyingine.

Hakukuwa na mzaha, lakini pale alipoamua kuutumia urembo wake kuinoigesha sinema hiyo hakuna mwanaume aliyeweza kuondoa jicho lake katika ‘screen’ kubwa zilizokuwa ikienea ukuta mzima katika majumba hayo ya sinema.

Mara nyingi umati wa mashabiki walionekana katika zile shoo zilizokuwa zikionyeshwa kuanzia saa 8:30 alasiri maana hapa ilijumuisha wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari wa kike na wa kiume.

Ilipokuwa kipindi cha likizo ilikuwa ni kazi kubwa sana kupata tiketi kuiangalia filamu hii ambapo kwa hapa Tanzania ilishamiri vilivyo miaka ya 1983 na kuendelea.

Inaaminika kwamba licha ya hivi sasa teknolojia kuongezeka duniani huku filamu zikiwa na ubora wa kipekee lakini bado waandikaji wa mikasa kama walivyokuwa akina Joseph Vila na Jonathan Demme bado ni wakutafuta sana.

Kijaruba kimeikumbuka filamu hii kwa vile ilileta kasheshe kiasi cha wavulana na wasichana kujikuta wakipenda kuwa na mahusiano na mtu aliyekuwa na rangi tofauti naye, mfano msichana mweusi alipenda kuwa na mvulana mweupe na hivyo hivyo kwa upande mwingine.

Wanafunzi wengi waliokuwa hasa na mapenzi ya filamu walitokea katika shule maarufu za Azania, Tambaza, Kinonondi Muslim, Kisutu, Kibasila, Zanaki na nyingine kadhaa za jijini Dar lakini kule Ashira, Marangu Girls, Kondoa Girs Tabora, Kiraeni na nyingine kadhaa nazo zilikuwa na wanafunzi waliozipenda filamu na kuwa wenyeji katika majumba haya ya filamu hasa katika vipindi vya likizo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.