Jinsi ya kupunguza gharama ya chakula cha kuku

Mtanzania - - Jiongeze - Na Grace Shitundu

UTAJIRI katika ufugaji unakuja endapo mfugaji anajiongeza na kutafuta maarifa kila kikicha ili mifugo yake iwe na tija.

Katika miaka ya karibuni watu wengi wamejitokeza kufanya ufugaji wa kuku wakiwa na tumaini la kupata faida na kuinua uchumi wa familia zao.

Baadhi ya wafugaji ambao walifanya mahojiano na JIONGEZE kwa nyakati tofauti wanasema kuna faida nyingi katika ufugaji wa kuku lakini pia kuna changamoto wanazokutana nazo zinazokwamisha malengo yao.

Wanasema moja ya changamoto ambayo imekuwa ikiwarudisha nyuma katika shughuli ya ufugaji wa kuku ni ulishaji yaani upatikanaji wa chakula.

Liliani Bukwimba ni mkazi wa Kinyerezi ambaye anafuga kuku wa kisasa anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni katika ulishaji.

Anasema bei ya vyakula vya kuku imekuwa haitabiriki kila wakati inapanda kwa kiwango cha juu hali inayowafanya waingie gharama kubwa katika ulishaji

“Chakula cha kuku imekuwa ni changamoto kubwa hasa vyakula vya viwandani hali inayofanya baadhi ya wauzaji kutengeneza vinavyotokana na vitu vya asili ambavyo nayo wanauza bei,”anasema.

Naye Ana Joseph mfugaji wa kuku anayeishi Mbezi Beach ‘Africana’ anasema kutokana na wafugaji wengi kushindwa kuhimili gharama za chakula cha viwandani wengi wamekimbili kwenye vyakula vya kutengenezwa kienyeji kwa marighafi zinazopatikana katika baadhi ya sehemu.

“Hii imekuwa ni fursa kwa baadhi ya wafanyabiashara, wanatengeneza chakula na kuwauzia wafugaji hata mimi kwa sasa nanunua chakula hicho ingawa najua namna ya kutengeneza nakosa muda,”anasema.

Mfugaji mwengine wa kuku alijitambulisha kwa jina Mama Dotto anasema biashara hiyo ya kuuza vyakula vya kutengeneza imeshikwa zaidi watanzania wenye asili ya visiwa vya Zanzibar.

“Mwenzangu ‘wapemba’ wameshika soko la kuuza vyakula na wanatupata kwa kuwa hatujui namna ya kutengeneza hicho chakula kitaalamu. Kwa upande wake mfugaji Ivan Magige anasema yeye alipoona bei ya vyakula vya kununua inapanda kila wakati aliamua kutengeneza chakula mwenyewe.

“Niliamua kutengeneza chakula cha kuku mwenyewe baada ya kuelekezwa na mfugaji mwenzangu, nikaona kuwa tunatumia fedha nyingi.

“Miezi miwili iliyopita nilikuwa nanunua kilo 50 ya chakula ambayo ni sawa na debe mbili na nusu kuanzia Shilingi 57,000 hadi 65,000 lakini sasa natengeneza chakula kwa shilingi 70,000 zinazotoa gunia moja sawa na debe sita,”anasema Magige.

Anasema anatengeneza chakula hicho kwa kuchanganya gunia la pumba, mashudu ya alizeti kilo 15, mashudu ya pamba kilo 12, paraza 20, chumvi, nusu, mifupa nusu, chokaa nusu na dcp nusu.

Kutokana na hali hiyo JIONGEZE kwa msaada wa mitandao mbalimbali inakupa maarifa ya utengenezaji wa chakula cha kuku na unaweza kupata faida kwa kulisha kuku na kuuza wa wale wasioweza kutengeneza kwa kutokujua au kwa kukosa muda.

Kuku bora ni yule anayekua vizuri bila magojwa, mnene na anayetaga mayai mengi kama ni wa mayai hivyo ni lazima apate chakula kingi chenye ubora unaotakiwa.

Wanatakiwa kupata vyakula vya kutia nguvu, vya kujenga mwili, vya kuimarisha mifupa vya kulinda mwili na maji.

Vyakula vinavyotia nguvu

Huwa asilimia 60 hadi 70 ya mchanganyiko chakula cha kuku navyo ni pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano, nafaka vile mtama , chenga

za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi, mimea ya mizizi kama muhogo, viazi vitamu na magimbi (mizizi inatakiwa kulokwa aukupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ya asili na wapewe asilimia 10 tu).

Pia kuna vinavyotoa mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kujenga mwili Huwa asilimia 20 hadi 30 nayo ni mashudu au makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya, korosho, na ufuta .

Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), mabaki ya samaki/ dagaa na nyama, vyakula asilia kama minyoo, mayai ya mchwa, masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine

Vyakula vya kuimarisha mifupa(madini)

Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kumuweka kuku katika hali ya afya njema.

Madini ya chokaa (calcium) na fosiforasi (phosphorus)ni muhimu ili kuku watage mayai yenye ganda gumu.

Viinilishe vya madini

vinavyotakiwa ni pamoja na Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa, chumvi ya jikoni, madini ya viwandani ya Di-calcium phosphate, magadi (kilambo). Vyakula vya kulinda mwili Hivi ni vyakula vya mbogamboga kama mchicha wa kulimwa au pori, chinese, kabeji pia samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa,

Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).

Jua ni muhimu kwa upatikanajii wa vitamini A na D

Kuchanganya chakula majumbani (home made ration): Hii ni njia inayotumika kuchanganya chakula kwa ajili ya kulisha kundi dogo la kuku na njia ambayo inaweza kutumiwa na wafugaji wadogowadogo.

VIFAA; Beleshi /

koleo(spade), Turubai/sakafu safi, Viinilishe, Viroba/Magunia kwa ajili ya kuhifadhia chakula kilichochanganywa.

Chakula kilichochanganywa kinaweza kuwekwa katika uzani wa kilo 25-kilo 50, au kilo 100.

Mchanganyiko

Vyakula vya kutia nguvu mwilini (Pumba za mahindi kilo 48, Pumba laini za mpunga kilo 26 hivyo jumla inakuwa kilo 74, vya kujenga mwili 9 (mashudu ya alizeti kilo 18, damu ya wanyama kilo moja, mabaki ya samaki/ dagaa kilo tatu jumla inakuwa kilo 22.

Vya kuimarisha mifupa (Madini) chumvi ya jikoni nusu kilo chokaa kilo mbili, poultry premix nusu kilo, unga wa mifupa kilo moja jumla inakuwa kilo nne. Namna ya kuchanganya Kwanza changanya vizuri vyakula vya madini ya , chokaa, chumvi na majivu ya mifupa huu ni mchanganyo namba moja.

Pili changanya mchanganyo huo na damu pamoja na samaki waliosagwa huu ni mchanganyo namba mbili.

Tatu mchanganyo namba mbili uchanganye na mashudu vizuri ambao utauita namba tatu.

Nne mchanganyo namba tatu umwage juu ya rundo la pumba iliyochanganywa (pumba ya mahindi na pumba laini ya mpunga) nyanganya vizuri.

Utunzaji

Weka kwenye viroba au magunia na kutunzwa ghalani (stoo) hakikisha ni pakavu hadi pale kitakapohitajika.

Chakula hakitakiwa kukaa muda mrefu na kilichoharibika wasipewe kuku kinaweza kuleta matatizo ya kiafya.

Vyakula vya ziada

Kuku viinilishe kama mchwa na mafunza au nafaka. Inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani tofauti na wanafugwa nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .

Pia kiasi cha chakula hutegemea mahitaji kutokana na uzito na uzalishaji, mfano kuku anayetaga na anayekua wanahitaji chakula kingi zaidi ya wale ambao hawatagi au wamekoma kukua.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.