Alizeti, mafuta na makapi yake ni mali-2

Mtanzania - - Jiongeze -

Hii ni sehemu ya pili inayoeleza utajiri uliojificha ndani ya kilimo cha alizeti. Katika sehemu hii tutaangalia uvunaji, ukaushaji na usindakaji wa zao hili.

UVUNAJI

Alizeti hukomaa kati ya miezi minne hadi sita tangu kupandwa hivyo unatakiwa kukagua kuanzia wakati huo.

Alizeti iliyokomaa hubadilika rangi kutoka njano kuelekea nyeusi. Viuwa navyo hubadilika rangi kutoka njano na kuwa kahawia na hunyauka.

Inaelezwa ni vyema kuvuna mapema kuepuka wadudu na wanyama waha Vifaa vinavyohitajika wakati wa uvunaji ni pamoja na kisu, vikapu, magunia, matenga ( kwa ajili ya kubebea),maturubai, mikeka, kichanja( kwa ajili ya kukaushia), matoroli, mikokoteni ya kukokotwa na wanyama, treka lenye tela au gari (vyombo vya kusafirishia). Alizeti huvunwa kwa kutumia mikono ambapo suke hukatwa kwa kutumia kisu au mashine.

Wakati wa kuvuna masuke ya alizeti huwekwa kwenye vikapu ambavyo hutumika kusombwa na kusafirishwa hadi mahali pa kukaushia.

UKAUSHAJI

Alizeti hukaushwa katika hatua mbili ambazo ni kukausha masuke na kukausha mbegu.

Ukaushaji wa masuke hufanyika kwa kutandanzwa katika kichanja, maturubai au sakafu lengo ni kurahisisha upuraji au upukutishaji wa mbegu.

Hatua hii hufanyika baada ya kuhakikisha masuke yamekauka vizuri. Ni muhimu kupiga masuke taratibu ili kuepuka kupasua mbegu.

Hatua ya pili ni ukaushaji wa mbegu ambazo hukaushwa juani kwa kutandazwa kwenye vichanja,maturubai, mikeka au sakafu, hakikisha mbegu zinafika unyevu wa kiwango cha asilimia nane. Ili kutambua mbegu ya Alizeti kuwa imekauka unatakiwa kufikicha na maganda yake yanapotoka kwa urahisi inadhihirisha kuwa zimekauka. Pia mbegu ziliizokauka hung’aa na unapozimimina kwenye chombo hutoa mlio.

ONDOA TAKATAKA

Ondoa takataka ikiwemo wadudu, mawe katika mbegu kwa kupepeta kwa kutumia ungo au mashine zinazoendeshwa kwa mkono, injini au umeme.

Mashine hizi zina uwezo wa kupepeta na kupembua kilo 60 hadi 350 kwa saa kutegemea aina ya mashine na ukubwa wa mashine yenyewe.

UHIFADHI

Alizeti maghala bora ikiwa ni kwenye nyumba ifungashwe kwenye magunia na yapangwe kwenye chaga kwa kupishanisha yakiwa umbali wa mita moja kutoka ukutani. Hakikisha wadudu kama panya hawaingii ghalani kuepusha upotevu wa mbegu za alizeti.

MATUMIZI YA MBEGU ZA ALIZETI

Mbegu za alizeti hasa zenye mistari zinaweza kuliwa baada ya kukaangwa au kukaushwa.

Pia zinatumika katika utengenezaji wa mikate. Mbegu za alizeti husindikwa kupata bidhaa ya mafuta.

USINDIKAJI KUPATA MAFUTA

Vifaa vinavyohitajika ni pamoja na mashine ya kukamulia mafuta, chujio safi, ndoo, vifungashio, sufuria, mizani, mbegu za alizeti, maji na chumvi.

Namna ya kukamua kwanza chagua mbegu bora za alizeti zianike kwenye jua kwa muda wa saa moja hadi mawili kisha kamua mafuta kwenye mashine.

Baada ya kukamua chuja mafuta kwa kitambaa au chujio na uyapime mafuta hayo kisha chemsha baada ya kuchanganya na chumvi na maji.

Katika lita 10 za mafuta weka lita moja ya maji na gramu 200 za chumvi, chemsha hadi maji yote yaishe halafu ipua acha yapoe, kisha chuja kwa kitambaa safi au chujio Fungasha kwenye vyombo safi na vikavu na vyenye mifuniko, weka lebo na hifadhi kwenye sehemu safi, kavu na yenye mwanga hafifu tayari kwa kuingia sokoni.

Kamwe usitupe mashudu yake kwa kuwa nayo ni malighafi nzuri ya chakula cha mifugo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.