Iluminatha: Joto la Dar ni fursa kwa kuuza Juisi ya Matunda

“Ni vizuri vijana wakifanya biashara hii haichagui jinsia kwa sababu ni kazi rahisi kutengeneza

Mtanzania - - Jiongeze -

KUNA usemi umezoeleka kwa wengi kwamba kuishi jijini Dar es Salaam pekee ni sawa na kuwa na elimu ya kidato cha sita.

Msemo huu unatokana na jiji hili kuwa na changamoto nyingi ambazo ukiweza kuzikabili unakuwa umeliweza jiji.

Inaelezwa siri ya kuliweza jiji la Dar es salaam ni kuwa na shughuli ya kufanya iwe ya kuajiriwa au kujiajiri.

Biashara ndogondogo ya vitu mbalimbali ndio shughuli ambayo imekuwa ikichagamkiwa na vijana wengi hapa jijini kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Kipindi cha hali ya joto huwa ni kirefu katika jiji la Dar es salaam, kijana yeyote mwenye maarifa hukitumia kama fursa.

Wapo wanaouza maji, soda na hata juisi za viwandani lakini wapo wanauza juisi ya matunda ambayo imekuwa ikipendwa na wengi.

Iluminatha Juma ni msichana wa miaka 23 ambaye anaongeza kipato chake kwa kufanya biashara ya kuuza juisi ya matunda.

Anasema huwa ananunua matunda ya jumla katika soko la Buguruni kuanzia shilingi 5,000 na yanaweza kumpatia faida ya shilingi 20,000 hadi 30,000 inategemea na msimu.

“Biashara ya juisi hapa Dar haisumbui kwa kuwa muda mwingi kunakuwa na joto hivyo biashara huwa inatoka.

Anasema yeye anakaa Tabata na huwa anatengeneza juisi na kuweka kwenye chupa zilizoisha maji na kuuza kwa shilingi 500.

“Juisi ninayotengeneza ni nzuri kwa kuwa nachanganya matunda ya aina isiyopungua tatu na hivyo kuleta radha ya kipekee.

“Nafanya hivyo kwa kuwa jiji hili pamoja na kwamba hakuna wakulima lakini haliishiwi matunda kwani kipindi chote cha mwaka naweza kupata matunda ya aina tofauti,” anasema.

Iluminatha anatoa ushauri kwa vijana wengine kufanya biashara hiyo na kuacha mawazo ya kufanya mambo yasiyokubalika katika jamii.

“Ni vizuri vijana wakifanya biashara hii haichagui jinsia kwa sababu ni kazi rahisi kutengeneza juisi, kuliko kuwa mwizi au kuuza mwili wako ili upate pesa.

Anasema biashara hiyo imemsaidia kuongeza kipato kwenye familia yake na lengo lake la baadae ni kuwa na mgahawa ambao atautumia kuuza vitafunwa, maziwa na juisi.

Wapo wanaouza maji, soda na hata juisi za viwandani lakini wapo wanauza juisi ya matunda ambayo imekuwa ikipendwa na wengi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.