MAUMIVU

Mtanzania - - Hadithi - Itaendelea Jumamosi ijayo...

CHUMBA cha mkutano kilikuwa kimya, wote tukiwa makini kumsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi. Hapakuwa na kelele kabisa, mara chache kulisikika sauti za watu wakijikohoza. Ulikuwa mkutano wa siri uliofanyika ofisini kwa Mkuu wa Kitengo, Moses Lupango.

Akili yangu haikuwa sawa asubuhi hiyo, kila nilipofikiria vifo vya ajabu ajabu vya wapelelezi, nilizidi kukosa amani. Ukiacha suala la kukoseshwa amani na vifo tata, pia nilikuwa namfikiria sana mke wangu mpenzi Ester. Ni mwanamke wa maisha yangu, aliyekuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Mara nyingi alikuwa akihitaji kuwa na mimi lakini majukumu ya kikazi yalinisababisha kukosa fursa ya kuwa naye karibu kila wakati kama mwenyewe alivyokuwa akipenda. Mambo haya mawili yalitosha kabisa kunifanya niwe mwenye mawazo mengi sana asubuhi hiyo.

“Bila shaka hakuna asiyejua jambo lililosababisha tukutane kwa mara nyingine asubuhi ya leo,” sauti ya bosi wetu Moses Lupango ilininasua mawazoni.

Wote tukatingisha vichwa kuashiria kwamba tulikuwa tunajua. “Kitengo chetu kinazidi kugubikwa na hofu, lakini tunashindwa kufahamu huyu Patrick amekuwa na nguvu za aina gani siku hizi? Anaweza kuua wapelelezi wote hao kwa muda mfupi kiasi hiki? Mwaka jana alimuua Peter, baadaye James, mwaka huu tena wakamteka Anna na kumkata Mabesha vipande vipande!

“Amekuwa na mtandao mkubwa sana. Lakini hata hivyo, hatuweza kukaa kimya kwa mauaji yote haya, lazima akili zetu zifanye kazi ili tuweze kumtia mikononi mwetu,” alisema akituangalia kwa zamu.

Zilikuwa habari mbaya sana kwa Kitengo chetu. Akili yangu ikarudi nyuma, nikaanza kumkumbuka Patrick ambaye tulizoea kumuita Patii. Alikuwa akifanya kazi nasi katika kitengo kimoja, tena ofisi moja, lakini ghafla akabadilika na kuwa muuaji hatari.

Patii alikuwa mpelelezi, lakini kumbe alikuwa akishirikiana na majambazi kuvamia sehemu mbalimbali na kufanya uhalifu. Alifanya hayo kwa siri kubwa na hakuna yeyote aliyegundua. Siku moja wakiwa wamevamia nyumba ya tajiri mmoja Mbezi, akiwa na majambazi aliokuwa akishirikiana nao, alikamatwa!

Hapo ndiyo mwanzo wa tatizo, Barongo ambaye ndiye aliyefanikiwa kumkamata, baada ya kugundua aliyekuwa amemkamata ni mpelelezi mwenzake, akaamua kupambana, mwisho wake akamuua Barongo. Kitengo hakikuwa tayari kukubaliana na unyama huo. Idara ikaanza upelelezi mara moja, Patii akasakwa!

Kitu cha ajabu kila aliyejaribu kumfuatilia, ilikuwa lazima afe! Hakuna mpelelezi hata mmoja aliyewahi kufanikiwa kumkamata Patii, lakini kitendo cha kufanikiwa kumuua Mabesha na Anna kwa wakati mmoja, kilitufanya tuamini kwamba Patii alikuwa amejizatiti sana.

“Mapambano bado yanaendelea, safari hii tumeamua kuwaagiza watu wawili kwa mara nyingine wawafuatilie, tunawaamini sana watu hao, hatuna hofu nao kabisa,” alipofika hapo akakaa kimya.

Kila mmoja akamtizama mwenzake. Patii alitisha! Kulikuwa na kila dalili kwamba alikuwa na kikosi imara, wanaotumia mbinu za kisasa kufanya mauaji. Lupango akanitupia macho, kisha akajikohoza kabla ya kuanza kuzungumza tena.

“Joel...” aliita jina langu akinitizama machoni.

“Ndiyo Mkuu!” Nikaitika kwa heshima.

“Wewe na Pius mnatakiwa kusafiri kumfuatilia huyu mwanaharamu kwa mara nyingine. Habari zilizopo ni kwamba Patii na washirika wake, wamehamishia makazi yao nchini Uingereza na kujificha huko.

“Mnatakiwa mfahamu kwamba, kitengo kimewaamini kwa kiwango kikubwa sana, tunatambua uwezo wenu vyema, tunaamini mtatuwakilisha vyema,” akamaliza Lupango.

“Ndiyo Mkuu!” Tukaitika kwa pamoja.

“Kila kitu kimeshaandaliwa, nendeni nyumbani kwa ajili ya maandalizi, safari yenu itakuwa jumatatu,” akasema na kuahirisha kikao. Nikahisi kifo kifo! *** Sikutaka kuonyesha tofauti yoyote nyumbani, namjua vizuri sana mke wangu hivyo nilipaswa kuwa makini na mtulivu kabla ya kumweleza kuhusu safari yangu ya Uingereza. Pengine isingekuwa tabu sana mimi kusafiri kwenda Uingereza au nchi nyingine yoyote, lakini tatizo linakuja katika sababu ya safari yangu!

Ester anafahamu vizuri juu ya vifo vya wapelelezi wenzangu vilivyotokea, tena vikionyesha uwezo wa juu kabisa wa mauaji ya kimafia, haikuwa rahisi kumweleza kwa haraka kiasi hicho. Nikaonyesha uchangamfu wangu wa siku zote.

“Sema mpenzi wangu, habari za kushinda?” Nikamsalimia kwa furaha.

“Salama, nafurahi kukuona mume wangu, lakini umenifurahisha zaidi kwa kuwahi kurudi! Vipi hujapitia baa leo?” Akaniuliza akiunda tabasamu la kichovu sana.

“Hapana, leo nahitaji muda mwingi kuwa na wewe mpenzi wangu wa moyo. Unajua Ester nawapenda sana...” nikamwambia kwa utani huku nikipapasapapasa tumbo lake.

“Unatupenda? Wangapi?!” Akaniuliza akibenua midomo yake.

“Wewe na mwanangu aliyepo tumboni...” nikamjibu kwa kifupi.

“Mwanaume una mambo wewe!” Akasema akideka.

“Mambo gani bwana! Haya tuachane na hayo, nina taarifa nataka kukupa mke wangu, najua hutazifurahia, lakini inabidi ukubaliane nazo!” Nikamwambia nikionyesha umakini.

“Hata usiposema nimeshajua...si kwenda kumfuatilia Patii? Joe, kama ni hiyo kazi ni bora ukaachana nayo kuliko kwenda kufa mume wangu! Nakupenda sana na hilo unafahamu, unafikiri nitawezaje kuishi bila wewe mpenzi wangu? Sikuruhusu kwenda kufuata kifo chako mume wangu...” Ester alisema akitokwa na machozi, ilionekana aliyoyasema yalitoka moyoni mwake. Nikakosa maamuzi! Maneno ya mke wangu yaliniuma sana, lakini pia ilibidi akili yangu ifanye kazi kuliko kawaida. Kwenda Uingereza kulimaanisha kutimiza majukumu yangu ya kazi, ambayo naipenda na niliapa kwamba sitaisaliti kamwe, hata hivyo nampenda pia Ester wangu na kukataa kwenda kungeonyesha mapenzi yangu kwake! Hapo nikashindwa la kufanya. Nikamtizama kwa muda mrefu sana nikitafakari namna ya kumtuliza, akili ilikuwa kama imekufa ganzi, maana nilikosa mamuzi kabisa. Ester alikuwa akitokwa na machozi. Sikutamani kabisa kumuona mke wangu akiendelea kulia, nikapeleka mkono wangu wa kuume usoni mwake, kisha nikaanza kumfuta machozi yake.

“Sitaki Joe, sitaki...” akasema akizidi kulia. “Kuna nini mke wangu?” “Unajua...” “Nini?” “Kwani ulivyokuja ulisemaje?” “Kuhusu nini?” “Wewe si umesema una habari unataka kuniambia, tena habari zenyewe umeshasema kuwa ni mbaya!” Akasema akionyesha umakini sana.

“Ndiyo Ester wangu, lakini sijakuambia bado!” Nikamwambia nikipapasa-papasa tumbo lake.

“Ni habari gani mbaya zaidi ya kuniambia umepangiwa kumfuatilia Patii?” Akaniambia kwa kujiamini sana.

Hapo sasa nikahisi huenda kuna mtu wa kazini alimpigia simu mke wangu na kumweleza juu ya safari yangu ya kwenda Uingereza. Nikawaza kwa makini. Ni nani anaweza kumwambia mke wangu juu ya safari yangu ya Uingereza? Sikupata jibu. Hata hivyo mtu pekee mwenye namba za mke wangu ni rafiki yangu Magongo, ambaye pia nilishamweleza mapema asimwambie mke wangu chochote.

Mapambano bado yanaendelea, safari hii tumeamua kuwaagiza watu wawili kwa mara nyingine wawafuatilie, tunawaamini sana watu hao, hatuna hofu nao kabisa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.